SERIKALI KUANGALIA UPYA MFUMO WA STEMPU ZA KIELEKTRONIKI
Na Eva Ngowi, Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imepanga kupitia upya matumizi ya Mfumo wa Stempu za Kielektroniki (ETS) baada ya watumiaji wa mfumo huo kulalamika kuwa unagharama kubwa na kuwasababishia hasara kubwa huku kukiwa na mifumo mingine inayofanya kazi kama hiyo lakini kwa gharama nafuu.
Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru aliyeongoza jopo la Wataalamu wa Wizara hiyo walipofanya ziara ya kikazi kutembelea viwanda vya kutengeneza bia vya Tanzania Breweries Ltd na Serengeti Breweries Ltd.
Bw. Mafuru alisema kuwa wakati wa ziara hiyo wamebaini kuwa kuna mifumo inayofanyakazi zinazofanana lakini mfumo unaotumiwa na Serikali kuzalisha stempu hizo za kieletroniki unagharama kubwa ukilinganishwa na mfumo mwingine unaotumia teknolojia ya Block Chain ambao hauna gharama kubwa.
“Tutawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili watuambie sababu za kutoona kile ambacho sekta binafsi inayotumia mfumo huo inakiona ili tuje na utatuzi wa kuwapunguzia gharama wazalishaji wanazotumia kuendesha mfumo huo, fedha ambazo zingekuwa sehemu ya mapato ya Serikali, alisema Bw. Mafuru.
“Kuna mahali tumeambiwa kuwa wawekezaji hawa wanalipia Mfumo huo hadi shilingi bilioni 22 kwa mwaka, ukichukua asilimia 30 ya sh. Bilioni 22 kwa mwaka ni karibu sh. Bilioni 6.6 hiyo ingekuwa ni kodi ambayo hivi sasa hatuipati kwa sababu ni sehemu ya gharama ya kulipia Mfumo huo” Alisema Bw. Mafuru
Alisema kuwa kuna hoja zilizoibuliwa na viwanda hivyo tangu mwaka 2016 na kwamba zilihitaji kujibiwa ama kutatuliwa na taasisi za Serikali na Wizara nyingine za kisekta ili kuchochea uwekezaji nchini.
Bw. Mafuru alisema nia hasa ya kufanya ziara hiyo ni kutimiza wajibu wa Wizara ya Fedha na Mipango katika eneo la kusimamia uchumi kwani maendeleo ya nchi pamoja na uchumi wake unategemea ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji na utoaji wa ajira kwa wananchi.
“Ziara hii imelenga kutuwezesha sisi kuelewa kwanza changamoto ambazo wenzetu kwenye sekta hii hasa sekta ya utengenezaji wa vinywaji, wanazipitia na kupata mrejesho kutoka kwao kuhusu sera za hivi karibuni za kibajeti ambazo tumezipitisha kupitia bajeti ya Serikali, Sheria ya fedha lakini pia utekelezaji wa ile blue print, ambayo mwaka huu Serikali imetekeleza kwa kiwango kikubwa kupitia marekebisho yaliyofanywa na Sheria ya Fedha ya 2022” alisema Bw. Mafuru
Alisema kuwa Wizara yake inafanya hivyo ikiwa ni jitihada ya kupata mrejesho na hatimaye waweze kujua mahali panapohitajika kuongeza jitihada, kurekebisha mapungufu yanayojitokeza na pia kuangalia mahali panapofanyika vizuri ili kuifungua uchumi wa nchi.
Aidha Bw. Mafuru alisema kuwa jambo muhimu ambalo ameliona ni kwamba taasisi nyingi za Serikali zinafanyakazi kivyake na kwamba zinahitajika juhudi za pamoja za kuunganisha mipango yao na kushirikiana kiutendaji ambako kutaongeza tija katika nchi.
Bw. Mafuru aliongeza kuwa ili kuongeza uwekezaji nchini inapaswa kuwawekea wawekezaji mazingira rafiki ya kuwa na uhakika kama mitaji yao iliyopo hapa Tanzania italindwa ili waweze kuleta mitaji mingine.
“Makampuni yote mawili tuliyoyatembelea leo yana mipango ya kuongeza uwekezaji wao nchini lakini kuna kitu kinang’ang’ania kwenye mawazo ikiwemo kutokuwa na uhakika kama mambo wanayoyalalamikia yamechukua miaka mitatu hadi minnne kushughulikiwa na kutokuwa na uhakika wa kuongeza hatma yao” Aliongeza Bw. Mafuru
Akizungumzia changamoto ya uhaba wa chupa za bia, kunakochangia uzalishaji wa bia kuwa chini kutokana na kuwepo kwa kiwanda kimoja pekee cha kuzalisha chupa hizo, Bw. Mafuru alisema Wizara itaangalia masuala ya kisera ili kuongeza uzalishaji wa chupa hizo.
“Tutaongea na Wenzetu wa Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji waweze kuangalia namna ya kuongeza kasi ya kupata wawekezaji watakaoweza kuwekeza katika eneo hilo kwa sababu kuna fursa na bahati nzuri fursa hii sio tu kwa soko la Tanzania bali zitauzwa hata nchi Jirani na kutuwezesha kupata fedha za kigeni. Alisema Bw. Mafuru
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano wa Kampuni ya TBL Bi. Lucia Mwamboka, alisema wana matumaini kwamba mazungumzo yaliyofanyika kati ya Timu ya Wizara ya Fedha na Mipango yataleta tija na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali ili kupanua wigo wa kodi.
Aliiomba Wizara kuyafanyiakazi mapendekezo yao haraka iwezekanavyo na ikiwezekana ifikapo mwezi Desemba Mwaka huu, majibu ya kupunguza gharama za uendeshaji wa Mfumo huo wa Stempu za Kieletroniki unaosimamiwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, yapatikane.
Naye Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, Bw. John Wanyancha alisema wamefarijika kwa ujio wa viongozi kutoka Serikalini hususan Wizara ya Fedha na Mipango kusikiliza malalamiko yao na kuona jinsi ya kuyafanyia kazi na kuamini kuwa ziara ya Serikali kwenda kuwasilikiliza wawekezaji ni njia nzuri ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya viwanda hapa nchini.
Alisema kuwa Sekta hiyo ya uzalishaji wa vinywaji imekuwa kinara katika uchangiaji kwenye eneo la kodi na Serikali itahakikisha inafanya jitihada za kutatua changamoto zao ili waendelee kuchangia kwa sehemu kubwa na waendelee kukua na kuongeza ajira na kuleta maendeleo ya kiuchumi ambayo ndiyo matarajio ya Serikali.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi wa Mahusiano Serengeti Breweries Ltd Bw. John Wanyancha (kushoto), kulia ni Kamishna wa Sera Bw. Elijah Mwandumbya wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (kulia ) Pamoja na timu ya Wizara ya Fedha na Mipango walipotembelea kiwanda cha Tanzania Breweries Ltd. (TBL) kushoto ni Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano TBL Bi. Lucia Mwamboka.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akizungumza na timu ya Tanzania Broweries Ltd. (hawamo pichani) wakati alipotembelea kiwanda chao jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akiwa kwenye majadiliano na timu ya kiwanda cha bia cha Tanzania Breweries Ltd (TBL) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni timu ya Wizara ya Fedha na Mipango na kulia ni timu ya TBL.
Kamishna wa Madeni Bw. Japhet Justine asikiliza majadiliano kati ya Timu ya Wizara ya Fedha na Timu Serengeti Breweries Ltd (hawamo pichani) yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kiwanda cha bia cha Serengeti Breweries jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Sera Bw. Elijah Mwandumbya asikiliza majadiliano kati ya Timu ya Wizara ya Fedha na Timu Tanzania Breweries Ltd (hawamo pichani) yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kiwanda cha bia chaTBL jijini Dar es Salaam.
No comments: