HALMASHAURI WILAYA YA IKUNGI YABAINI MBINU MPYA UKUSANYAJI WA MAPATO

Kikao kikiendelea. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma ya Jamii, ambaye ni Diwani wa Kata ya Siuyu, Selestine Yunde, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Halima Ng'imba na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Diwani wa Kata ya Muhintiri, Hamisi Mpuma.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza na Madiwani wa halmashauri hiyo wakati akifungua kikao cha kawaida cha baraza la madiwani ambacho ni cha mwisho wa mwaka kilichoketi leo Septemba 6, 2022 wilayani humo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Petro Mtyana na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Justice Kijazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akizungumza kwenye kikao hicho.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Petro Mtyana akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Mika Likakapa akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya maafisa watendaji na wataalamu wa halmashauri hiyo wakiwa kwenye kikao hicho.

Kikao kikiendelea.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa kikao hicho. Kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Ikungi, Stamili Dendego na kulia kwake ni Katibu wa Chadema wa wilaya hiyo, Ibrahim Saidi.
Kikao kikiendelea.
Wakuu wa idara na wataalam wa halmashauri hiyo wakiwakwenye kikao hicho.
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Makiungu, Zainabu Hamisi akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Diwani wa Kata ya Isuna, Stephano Misai akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Taswira ya kikao hicho.
Diwani wa Kata ya Iyumbu Peter Kweligwa akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika kikao hicho.
Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Mungaa, Hellen Petro akizungumza kwenye kikao hicho.
Diwani wa Kata ya Mtunduru, Ramadhani Mpaki akizungumza.
Diwani wa Kata ya Ntuntu (CHADEMA), Omari Toto akijibu maswali ya madiwani yaliohusu ukusanyaji wa mapato.
Diwani wa Kata ya Unyahati, Abel Suri akichangia jambo kwenye kikao hicho.

Na Dotto Mwaibale, Ikungi
HALMASHAURI yaWilaya ya Ikungi mkoani Singida imeanza mkakati mpya wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato wenye lengo la kuongeza mapato baada ya chanzo chao kikubwa cha mazao ya biashara kuporomoka kutokana na uhaba wa mvua.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga wakati akifungua kikao cha kawaida cha baraza la madiwani ambacho ni cha mwisho wa mwaka kilichoketi leo wilayani humo.

"Tumekwisha ingia mwaka mpya wa fedha na kama mnavyojua kuwa jiografia ya halmashauri yetu mvua zikinyesha chini ya kiwango zinasababisha mazao kupungua kama vile alizeti, mpunga, dengu na mazao mengine" alisema Mwanga.

Alisema baada ya kutokea hali hiyo walishauriana kuangalia vyanzo vya mapato vya uhakika ambavyo vitaisaidia halmashauri hiyo kukusanya mapato na kuwa mpango wa kwanza utaanzia Stendi ya mabasi ya Kata ya Mungaa ambapo kama watasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato baada ya magari kuingia katika stendi hiyo kwa mwezi watapata Sh. 16 Milioni na zaidi ya fedha hiyo.

Mwanga alisema maeneo mengine watakayo yaangalia ni stendi ya mabasi ya Isuna, Ikungi, Ihanja, Sepuka na maeneo mengine yanayofananana na hayo na kufungua minada Kijiji cha Choda na Chungu jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.

Alisema kuacha magari yakipita bila ya kuweka utaratibu wa kuingia stendi zitakazoanzishwa itakuwa ni hasara kwa halmashauri hiyo ambapo alitumia nafasi hiyo kuziomba kila kata yanapopita magari hayo ni lazima watengeneze stendi hizo.

Mwanga alitaja vyanzo vingine wanavyotarajia kuvianzisha kuwa ni pamoja na kufungua minada maeneo mengine ndani ya halmashauri hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alisema anakubaliana na mkakati wa madiwani hao wa kuanzisha mpango huo kabambe wa kuwa na vyanzo vya mapato na akasisitiza kuwa wakipata maeneo ya kuweka stendi hizo halmashauri itasaidia kupeleka katapila la kutengeneza maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kujenga vyoo.

Halikadharika Kijazi alisema mwaka wa fedha uliopita wa 2021/ 2022 halmashauri hiyo imeweza kufikia asilimia 102 ya kukusanya mapato lakini akasisitiza kuwa itakuwa haina maana kukusanya mapato kwa wingi na matumizi yakawa ni makubwa na kueleza kuwa wanakwenda kuondoa posho zisizo za lazima na fedha hizo watazielekeza kwenye miradi ya kupata fedha zaidi.

Alisema mafanikio ya kufikia asilimia hiyo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya madiwani na watumishi wa kada nyingine wa halmashauri hiyo na lengo likiwa ni kuiletea maendeleo.

Katika hatua nyingine Kijazi aliliomba baraza hilo la madiwani kupitisha Sh.100 Milioni kwa ajili ya kuifunga stendi ya mabasi ya Ikungi akitolea mfano stendi ya Manyoni ambayo kila siku wanakusanya Sh.Milioni 3.5 mabasi yanapopita hivyo ikifunguliwa wataweza kupata Sh. Milioni 3 hadi 4.

Aidha Kijazi alisema watendaji wote watakao onekana wakilegalega katika suala zima za ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yao watawaondoa.

Diwani wa Kata ya Unyahati, Abel Suri alisema uanzishaji wa vyanzo hivyo vya mapato ni jambo la lazima ambapo aliomba ufanisi na nguvu katika ukusanyaji wa mapato hayo iongezeke hasa kwa watendaji wa kata.

"Tunawaomba watendaji wote wa kata wawajibike na kuongeza bidii ya kukusanya mapato kwani hiyo ni moja ya kazi yao kubwa na hata katika mkataba wao wa kazi jukukumu hilo lipo" alisema Suri.

Suri alisema moja ya kipimo cha utendaji kazi wa maafisa hao ni ukusanyaji wa mapato na si vinginevyo.

Katika kikao hicho ajenda kubwa ilikuwa kila kata kutoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ambapo kata nne zilizofanya vizuri zilitoa taarifa halikadharika kata nne ambazo zilizofanya vibaya nazo zilitoa taarifa na sababu zilizojitokeza mpaka zikafanya vibaya na hatua zitakazofanyika ili kuongeza mapato.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Mika Likakapa ambaye alikuwa mgeni mualikwa katika kikao hicho alisema madiwani hao wanapaswa kuzingatia vyanzo vya mapato vikubwa na si vile vidogo vidogo ambavyo vinaweza kuwaletea wananchi usumbufu na kuleta changamoto.

No comments: