DKT. STERGOMENA: MATISHIO YA AMANI NA USALAMA NI KICHOCHEO CHA UTAFITI NA UBUNIFU

 

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amesema kuwa matishio ya Amani na Usalama yameendelea kubadilika muda wote, na hivyo kuongeza umuhimu wa utafiti pamoja na ubunifu unaokwenda sambamba na kasi wa ukuaji na mabadiliko ya kiteknolojia duniani, ambapo zana na vifaa vinabadilika na kuhitaji kuhuishwa kulingana na mahitaji ya wakati.

Aidha, Dkt. Stergomena amebainisha kuwa kulingana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia ulimwenguni, ni muhimu sana kukidhi mahitajio ya kiteknolojia kwa Jeshi na Taifa kwa ujumla. Hivyo basi ni vyema kuendelea kufanya tathmini na tafiti endelevu ili kuona mahitaji na mipango inaendana na maendeleo ya kiteknolojia pamoja na kusimamia na kujitegemea kikamilifu.

Waziri Stergomena ameyasema hayo alipoongea Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma, wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Shirika la Tanzania Automotive Technology Centre (TATC) maarufu Nyumbu Project. Madhumuni ya ziara hiyo, yakiwa ni kufahamiana na watumishi wa Shirika pamoja nakuzifahamu vyema shughuli mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa katika Shirika hilo.

Dkt. Tax kwa umuhimu wa kipekee amesifu na kupongeza kazi nzuri na ya kitaalamu inayoendelea kufanywa katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Shirika. Kwa sehemu kubwa majukumu haya yanahusiana na utafiti, uvumbuzi, uhawilishaji teknolojia na uundaji wa zana, mitambo na vipuri mbalimbali vinavyotumika katika Jeshi letu na katika Taasisi mbalimbali za kiraia.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, kufuatia ndoto za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, likiwa na lengo la kuendeleza mapinduzi ya teknolojia za magari nchini kwa kufanya utafiti na ubunifu ili Taifa liweze kujitegemea kiteknolojia. Shirika hili limeendelea kufanya tafiti mbalimbali na kubuni na kutengeneza mitambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na magari ya Nyumbu, vifaa vingine kama vile spea kwa ajili ya mitambo na mashine mbalimbali.

Vile vile, Mheshimiwa Waziri ametoa rai kwa watendaji wa Shirika hili, kujikita zaidi kwenye ubunifu wa zana na vifaa vya kijeshi vinavyohitajika katika karne hii ya 21, hususan vitakavyowezesha kukabiliana na matishio ya sasa na yatayojitokeza. Hali hii inahitaji kuongeza nguvu zaidi katika maeneo mengine katika kujenga uwezo wa Shirika kiutafiti na kiubunifu katika maeneo stahiki, kukuza ushirikiano na Taasisi nyingine za utafiti na ubunifu.

Kuhusu Mpango wa Maendeleo Miaka wa Kumi 2021/22 – 2030/31 wa Kuliimarisha Shirika ili liweze kutekeleza majukumu yake ya utafiti na uhawilishaji teknolojia ya magari, utakaogharimu takriban Shilingi bilioni 75.4, Mheshimiwa Waziri amewahakikishia kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla, zitahakikisha kuwa Mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi katika kuliwezesha Shirika kukidhi azima ya kuanzishwa kwake.

Aidha, Dkt. Stergomena ameongeza kusema kuwa Serikali inayo nia njema ya kuliwezesha Shirika kwa kutafuta rasilimali za ziada, zikiwemo kuingia ubia na wawekezaji wenye uwezo na nia thabiti katika kudumisha ulinzi na amani ya Taifa letu. Kwani mataifa yaliyoendelea, sekta binafsi ni mbia muhimu sana katika uzalishaji wa zana na vifaa vya kijeshi, hivyo basi kuwapata wabia stahiki nayo pia ni sehemu ya ubunifu.

Kabla ya kuhitimisha hotuba yake, Mheshimiwa Waziri alifikisha salaam za Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuwa anatambua na kuthamini kazi kubwa na ya kizalendo inayoendelea kufanywa na Shirika. Aidha, anatambua umuhimu wa Shirika la Nyumbu kwa Jeshi letu na Taifa kwa ujumla.

Amewahakikishia watumishi hao pia, kuwa Amiri Jeshi Mkuu anayo dhamira ya dhati katika kupunguza na hatimaye kuzimaliza kabisa changamoto zinazowakabilia. Kwa maana hiyo, akawataka waandelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuchapa kazi kwa utii, uhodari na uaminifu kama vilivyo viapo vyao na umahiri, ubunifu na kwa na kwa ufanisi huku wakiweka mbele maslahi mapana ya Taifa.

No comments: