MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA JUKWAA LA WAKULIMA KIGALI RWANDA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akihutubia katika Jukwaa la Wakulima kwenye Mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika wa mwaka 2022 (AGRF 2022) unaofanyika Kigali nchini Rwanda. Tarehe 06 Septemba 2022
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akisikiliza wazungumzaji mbalimbali katika Jukwaa la Wakulima kwenye Mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika wa mwaka 2022 (AGRF 2022) unaofanyika Kigali nchini Rwanda. Tarehe 06 Septemba 2022

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema ili kuharakisha mabadiliko katika mfumo wa Chakula, Mataifa ya Afrika yanapaswa kuweka sera rafiki katika sekta ya kilimo zitakazorahisisha upatikanaji zaidi wa fedha kwa vijana na wanawake ili waweze kuvutiwa kushiriki katika kilimo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akitoa hotuba katika Jukwaa la Wakulima kwenye Mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika wa mwaka 2022 (AGRF 2022) unaofanyika Kigali nchini Rwanda. Ameongeza kwamba inapaswa kuweka kipaumbele katika ufadhili wa tafiti na maendeleo pamoja na huduma za ugani zitakazosaidia katika kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na hivyo kuhakikisha usalama wa chakula. Amesema ni muhimu ufadhili huo ukalenga uendelezaji wa rasilimali watu, kuvumbua mazao mapya pamoja na kukuza teknolojia rafiki kulingana na mazingira husika.

Halikadhalika ameongeza kwamba viongozi wa serikali pamoja na sekta binafsi hususani wanaosimamia sekta ya kilimo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kwenye kilimo ili wawe mfano kwa wakulima wengine na pia chachu ya utengenezaji wa sera rafiki za kilimo. Pia amesema ni muhimu kusimamia matumizi ya mizani na vipimo ili kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji unaojitokeza katika masoko ya mazao yao.

Makamu wa Rais amesema Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kilimo ili kuwa na uhakika wa chakula ikiwemo ajenda ya “10/30 kilimo ni biashara” inayolenga kukuza sekta hiyo kufikia asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030 ambapo katika kufikia hayo serikali inaendelea kuhamasisha sekta ya umma na binafsi kuwekeza katika kilimo, kuongeza bajeti ya kilimo, kutumia teknolojia ya kidijitali kwaajili ya kupanga,kufuatilia na kutathimini huduma za ugani,masoko na malipo.

Aidha amesema kupitia ushirikiano wa kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika(SADC), Tanzania imeendelea kurahisisha mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo kwa kuondoa ushuru na vikwazo mbalimbali vya kiforodha na visivyokuwa vya kiforodha,kuondoa vikwazo vya usafirishaji mazao nje ya nchi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa habari kwa nchi washirika katika biashara hiyo.

Makamu wa Rais yupo nchini Rwanda kuwamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika wa mwaka 2022 (AGRF 2022).

No comments: