SERIKALI YA AWAMU YA SITA INAVYOWAJALI NA KUWATHAMINI WASTAAFU
*Waziri Ndalichako asema dhamira ya Rais Samia ni kila mstaafu kupata haki yake, atoa maagizo mazito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango kwa wakati
Na MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amewahakikishia wastaafu nchini kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutatua changamoto zinazowakabili wastaafu nchini.
Waziri Ndalichako alisema hayo leo Jijini Mwanza ikiwa ni muendelezo wake wa kukutana, kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wastaafu ambapo tayari alishakutana na wastaafu wa Jiji la Dodoma na Dar es Salaam.
Alisema Rais Samia anawajali na kuwathamini wastaafu wote nchini kutokana na mchango wao mkubwa walioutoa katika ujenzi wa uchumi wa nchi na ndio maana anataka kila mtumishi anayestaafu alipwe haki yake kwa mujibu wa Sheria.
“Ndio maana nimeanza kukutana na wastaafu wetu kwani haya ni maelekezo ya Mhe. Rais Samia ambaye anawapenda sana wazee wastaafu wetu hivyo nimekuja hapa Mwanza kusikiliza na kutatua kero zao,” alisema.
Waziri Ndalichako alitoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati kwani baadhi ya kero za wastaafu zinasababishwa na waajiri kutowasilisha michango kwa wakati.
Alisema kutokana na hali hiyo Wizara anayoisimamia itahakikisha inafanya kaguzi za mara kwa mara ili kuwabaini waajiri wote ambao hawawasilishi michango na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria.
“Waajiri wote wasimamie sheria bila shuruti kwa sababu sheria iko wazi mfanyakazi anakatwa asilimia kumi na mwajiri anaongeza asilimia kumi inapatikana asilimia 20 ambayo itawasilishwa kwenye mifuko,” alisema.
Aidha, Waziri Ndalichako aliwaomba watumishi wote wa Sekta binafsi na Umma kuwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ina mifumo ambayo inawawezesha kufuatilia michango popote walipo kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ambapo kupitia simu ya kiganjani mtumishi anaweza kuona taarifa zake.
Alisema kwa upande wa watumishi wa umma Serikali imeona tatizo la baadhi ya waajiri hasa wa halmashauri kutowasilisha michango ambapo kuanzia mwezi Julai mwaka 2022 Serikali ilichukua ya kukata moja kwa moja michango ya watumishi.
Waziri Ndalichako alisema baadhi ya changamoto za wastaafu ambazo amezibaini katika Jiji la Mwanza ni mapunjo ya mafao kwamba mstaafu alilipwa tofauti na kile alichopaswa kulipwa kulingana na michango yake au mshahara wake.
Alisema changamoto nyingine ambayo ameibaini ni baadhi ya waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa NSSF na PSSSF jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri Ndalichako aliwashukuru wastaafu wa Jiji la Mwanza kwa muitikio mkubwa ambapo aliwaagiza wakurugenzi wakuu wa PSSSF na NSSF kuendelea kuweka mifumo na utaratibu wa kuwasikiliza kero za wastaafu.
“Tuendele kuimarisha mifumo ya kuwahudumia wateja wetu ili wastaafu hawa ambao wamelitumikia Taifa hili kwa weledi na moyo wao wote basi wanapostaafu wapate haki zao kwa wakati,” alisema.
Naye, mstaafu Zaina Mussa alimshukuru Waziri Ndalichako kwa kusikiliza kero za wastaafu na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
“Tunakuomba mheshimiwa Waziri tufikishie salamu zetu kwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotujali na kututhamini,” alisema.
Naye, Nyamsonga Alfed alisema kitendo kinachofanywa na Waziri Profesa Ndalichako cha kukutana na kusikiliza kero za wastaafu ni cha kihistoria kwani kinaleta majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Huduma inayotolewa katika mkutano huu wa Waziri Profesa Ndalichako ni nzuri kwani anasikiliza kero za wastaafu mmoja mmoja na kuzipatia ufumbuzi wa haraka,” alisema Godfrey Anton.
No comments: