Benki ya NMB yaendelea kuwa kinara wa ufanisi nchini Tanzania
Kwa Ufupi: Benki ya NMB yaendelea kuwa kinara wa ufanisi nchini Tanzania. Faida ya benki kabla ya kodi yafikia TZS bilioni 298, sawa na ongezeko la asilimia 54.
· Faida baada ya kodi: TZS bilioni 208 - ongezeko la asilimia 53 kwa mwaka
· Jumla ya Mapato ya benki: TZS bilioni 562- ongezeko la asilimia 21 kwa mwaka
· Jumla ya Mali: TZS Trilioni 9 - ongezeko la asilimia 19 kwa mwaka
_________________________________________________________________
Dar es Salaam. July 28, 2022- Benki ya NMB imeendeleza ufanisi wake kiutendaji katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022. Faida kabla ya kodi imeongezeka kwa asilimia 54 na kufikia Shilingi bilioni 298 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 193 ya kipindi kilichoishia June 2021. Faida baada ya kodi imeongezeka kwa asilimia 53 na kufikia Shilingi bilioni 208 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 135 ya kipindi kilichoishia June 2021. Faida hii inatokana na kuongezeka kwa ufanisi, kukua kwa mizania ya benki, ubora na umakini katika kusimamia mikopo, na kuongezeka kwa miamala ya wateja.
Mapato ya Benki yameongezeka kwa asilimia 21 hadi kufikia shilingi bilioni 562 katika kipindi kilichomalizikia mwezi Juni 2022 ikilinganishwa na shilingi bilioni 463 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka jana. Mapato haya yamechangiwa na ongezeko la mikopo kwa wateja na uwekezaji kwenye hati fungani za Serikali, pamoja na ongezeko la miamala ya kibenki.
Benki imeendelea kuimarisha ufanisi kwenye gharama za uendeshaji, ulioshuhudia uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato ukishuka mpaka asilimia 42 kutoka asilimia 47 katika kipindi kama hichi mwaka uliopita. Benki imeendelea kutilia mkazo uimarishaji wa ufanisi huku ikiboresha uwekezaji katika teknolojia na vipao mbele vya kimkakati vyenye lengo la kuongeza ubora wa huduma za kibenki.
Katika kipindi hiki cha nusu ya mwaka 2022, ubora wa mali za NMB uliimarika kutokana na mikakati thabiti ya kuimarisha mikopo ya benki. Uwiano wa mikopo chechefu umeimarika hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.3 katika kipindi kama hiki mwaka uliopita, ikiwa ndani ya kiwango cha juu cha asilimia 5 kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Katika kipindi hiki cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022, Mizania ya Benki iliongezeka kwa asilimia 19 na kufikia Shilingi Trilioni 9, ukilinganisha na Shilingi Trilioni 7.6 kutokana na kuongezeka kwa wateja, ikiashiria ubora na mahusiano mazuri ya benki na wateja wake.
Akizungumzia mafanikio haya makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema: “Tunajivunia na kushukuru kwa ufanisi na uimara wa benki yetu ya NMB. Mafanikio haya makubwa ya nusu ya mwaka 2022 ni kielelezo cha ufanisi mzuri uliotokana na utekelezeji makini wa mikakati yetu. Tunayo furaha kuona benki ikiendelea kupata matokeo mazuri na endelevu ya kiutendaji yenye kuleta tija kwa wanahisa wetu, wateja wetu, na wadau wote wa Benki ya NMB.”
Aliongeza kwa kusema kuwa: “Tutaendelea kuimarisha na kujikita katika misingi yetu imara, pamoja na kutilia mkazo uwekezaji katika teknolojia, pamoja na uboreshaji wa huduma zetu ili kuhakikisha benki inaendelea kupata mafanikio endelevu zaidi na yenye kuleta maendeleo chanya kwa Taifa.”
Aidha, Bi Ruth alimalizia kwa kusema, ‘Tunawashukuru wateja wetu, wafanyakazi, wawekezaji, na wadau wote nchini Tanzania, kwa mchango wao mkubwa katika mafanikio haya ya Benki ya NMB.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna
No comments: