Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho akizungumza na kaya 644 za makazi ya Magomeni kota na kuwahakikishia kuwa wataishi bure kwa miaka mitano kwa mujibu wa ahadi ya Rais Hayati. John Joseph Magufuli, leo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Mbunifu Majengo Daud Kondoro akizungumza wakati wa kikao maalum kilichomkutanisha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na kaya 644 za Magomeni kota kikao kilichofanyika katika makazi hayo leo jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wakazi wa Magomeni kota akitoa shukrani kwa niaba ya wakazi hao na kumshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwahudumia watanzania na kumwomba kuja kuzindua na kukabidhi funguo kwa mpangaji wa kwanza wa makazi hayo, Leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa mtaa wa Magomeni kota George Abel akizungumza katika kikao hicho ambapo amemshukuru Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa kutoa sitofahamu kuhusu uhalali wa wapangaji watakaorejea kwenye makazi hayo, leo jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya wakazi wa Magomeni kota wakifuatilia mkutano huo.
WAZIRI Wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho amewahakikishia wakazi 644 waliokuwa wakiishi katika eneo lililojengwa nyumba za kisasa Magomeni kota kuwa, kaya zote zilizokuwa zikiishi hapo awali zitarejea katika nyumba hizo zilizojengwa kwa fedha za Serikali na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA.) Na wataishi katika nyumba hizo kwa miaka mitano bure kama ilivyohaidiwa na na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Hayati Dkt. John Joseph Magufuli na sasa Serikali ya Rais Samia ambayo haijabadili ahadi hiyo.
Akizungumza na kaya 644 zilizokuwa zikiishi katika eneo hilo leo jijini Dar es Salaam Waziri Chamuriho amesema, hadi kufikia mwezi Oktoba nyumba hizo zitakuwa zimekamilika na kaya zote 644 zitaingia katika makazi hayo mapya na kuwataka kupuuza habari zinazoenea zikieleza mabadiliko ya wakazi wapya wa maeneo hayo.
''Nyumba hizi ni kwa ajili ya kaya 644 kama ilivyoelekezwa na Rais, na kuna ongezeko na kaya 12 ambazo zitatumika kwa matumizi maalumu ikiwemo uongozi na utawala hivyo nitoe rai taarifa sahihi zinazotolewa na Serikali kuhusu makazi haya zinatolewa na Wizara na TBA na si vinginevyo hivyo, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inawatambua wakazi 644 watakaoingia na kuishi katika makazi haya.'' Amesema.
Amesema kuwa baada ya wakazi hao kupeleka taarifa zao za uhakiki Wizara inaendelea na zoezi la uhakiki wa taarifa hizo na wategemee kuishi katika makazi hayo kwa mujibu wa ahadi ya Rais kwa kuishi katika makazi hayo kwa miaka mitano bure na watachangia gharama za huduma muhimu ikiwemo ulinzi, huduma jumuishi za usafi, maji, umeme na michezo ya watoto ambazo kwa sauti moja wakazi hao walikubali kuchangia huduma hizo muhimu.
Vilevile Waziri Chamuriho amesema miongozo na mikataba vinaandaliwa na watakabidhiwa siku ya kuingia katika makazi hayo na kuwataka kujiandaa kulinda mali ya Umma iliyojengwa kwa gharama kubwa na Serikali na kukamilika kwa asilimia 99 hasi sasa.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao Semvua Ayoub amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwatumikia watanzania na kumwomba kuja kuzindua makazi hayo na kukabidhi funguo kwa mpangaji wa kwanza wa makazi hayo.
No comments: