SHIRIKA LA POSTA LAIBUKA KIDEDEA AFRIKA, WAZIRI MKUU KUZINDUA HUDUMA YA ONE STOP CENTRE
Na Zainab Nyamka, Michuzi TV
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile amesema Shirika la Posta Tanzania limeshinda katika vipengele viwili na kuibuka kidedea kwenye upande wa Baraza ya utawala na Baraza la uendeshaji kwa kupigiwa kura na mashirika ya Posta duniani.
Dkt Ndugulile amesema Posta ya Tanzania imeibuka kidedea baada ya kushindanishwa na mashirika ya Posta mbalimbali Afrika na kuaminiwa katika utoaji wake wa huduma.
Hayo ameyasema leo Jijini Dar es Salaam na kusema kuwa wizara yake ndiyo inayosimamia mabadiliko ya kidijitali kwa upande wa TEHAMA kuanzia sekta za fedha, mitandao na mifumo ya kiusalama ya mtandao huku Tanzania ikiwa ni ya pili baada Mauritius.
Akizungumza kuelekea uzinduzi wa Huduma kwa pamoja (One stop Centre), Dkt Ndugulile amesema huduma mbalimbali za kiserikali zitakuwa zinapatikana katika ofisi za Shirika la Posta na zitamrahisishia mwananchi kuweza kupunguza mzunguko wa kwenda kwenye ofisi zao.
Katika uzinduzi huo utakaofanyika siku ya Jumatatu Septemba 06 mwaka huu , Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa kuzindua tukio hilo muhimu ya huduma pamoja ( one stop centre).
Dkt Ndugulile amesema Mikakati iliyopo ni kuendelea kutoa huduma na kuongeza taasisi zingine katika mfumo huo wa Huduma pamoja ambao unaenda kuondoa mfumo wa kizamani na kuingia kidigitali utakaomuwezesha mwananchi kupata huduma ndani ya ofisi moja ya Shirika la Posta na rasmi inaenda kuzinduliwa.
“Huduma hii inaenda kuzinduliwa rasmi na tunashukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekubali kuwa mgeni rasmi na huduma hii inaanza kwa awamu na utaanzia Dar es Salaam na Dodoma na kisha baadae itasambaa kwenye Mikoa mingine kwa awamu tofauti,” amesema.
Dkt Ndugulile amesema, Tanzania inaendelea kuboresha huduma zake katika upande wa Shirika la Posta na kuongeza wigo wa huduma na kufikia malengo makubwa ya kidigitali ndani na nje ya nchi.
Amesema, Moja kazi kubwa inayofanywa na wizara yake ni kuona Shirika la Posta Tanzania linaenda katika mfumo mpya wa kidigitali kuanzia muonekano wake hadi huduma zake.
Akizungumzia huduma zilizoboreshwa ndani ya Shirika la Posta, Kaimu Postamasta Mkuu Macrice Mbodo amesema toka kuzinduliwa kwa Duka mtandao Shirika la Posta limeweza kuingiza faida ya mil 300.
“ mfanyabiashara anapojiunga katika huduma ya duka mtandao na kuuza bidhaa zake sisi kama Shirika la Posta tunapata asilimia 3 ya bei ya bidhaa sambamba na gharama za usafirishaji na hilo limepelekea Shirika kupata milion 300 toka kuzinduliwa kwake,” amesema.
Mbodo amesema, bado Shirika lake linaendelea kuboresha huduma na kwa sasa linaendelea kutengeneza faida na kwa mwaka wa fedha ulioisha limeingiza faida ya Bilion 3 na mabadiliko ya mfumo wa kidigitali yataenda kwa awamu tatu ambapo Kufikia Desemba 2022 mikoa isiyopungua 10 itakuwa imepata huduma ya pamoja kwa ofisi zote za kiserikali kuwa katika ofisi moja.
“Tunaanza na Mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma, tutaenda Mwanza, Kigoma, Arusha, Mbeya, Zanzibar, Mji Magharibi, Chakechake Pemba,, Lindi, Tanga na Morogoro na awamu ya pili itaanzia 2023/24 itakuwa katika mikoa ya
Pwani, Iringa, Rukwa, Ruvuma, Kilimanjaro, Tabora, Mara, Kagera, Shinyanga, Lindi, Simiyu, Mtwara, Manyara, Songwe,Katavi, Njombe na Geita,” amesema Mbodo
Aidha, ameongezea na kusema kufikia Desemba 2025 Shirika la Posta limejizatiti kufikisha huduma ya Pamoja kwa ngazi ya wilaya ili kuwafikia wananchi zaidi.
Posta Tanzania inazindua rasmi huduma ambayo itazikutanisha taasisi mbalimbali za kiserikali kutoa huduma kwa pamoja ikiwemo Brela, NSSF, RITA, Uhamiaji, PSSF na zinginezo ambazo zitatoa huduma kwa pamoja.
No comments: