TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUFANYA MIKUTANO YA MABARAZA YA WAFANYAKAZI KUJADILI NAMNA BORA YA KUTEKELEZA BAJETI YA 2021/22



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (katikati) akizungumza na Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI lililofanyika katika Ukumbi wa TAFORI Mjini Morogoro.


Baadhi ya Wajumbe waliohudhuria Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza hilo uliofanyika katika Ukumbi wa TAFORI Mjini Morogoro.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kuzungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI lililofanyika katika Ukumbi wa TAFORI Mjini Morogoro.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kufungua Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais-UTUMISHI uliofanyika katika Ukumbi wa TAFORI Mjini Morogoro.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Ofisi ya Rais- UTUMISHI mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika katika Ukumbi wa TAFORI Mjini Morogoro.

 

Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka Taasisi za Umma kufanya mikutano ya Mabaraza ya Wafanyakazi ili kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 iliyoidhinishwa na Bunge kwa lengo la kujadili namna bora ya utekelezaji wa mpango kazi wa bajeti hiyo kwa kuzingatia mtiririko wa fedha.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la ofisi yake uliofanyika mjini Morogoro kwenye Ukumbi wa TAFORI.

Mhe. Mchengerwa amesema, Mabaraza ya Wafanyakazi katika taasisi zote za umma yapo kisheria, hivyo yanapaswa kuwa hai katika kupokea na kujadili bajeti za taasisi zao na kuongeza kuwa, kwa kufanya hivyo taasisi zitaimarisha ushirikishwaji wa watumishi katika kutekeleza majukumu ya Taasisi za Umma.

 Akizungumzia mchango wa ofisi yake katika kujenga Taasisi za Umma imara, Mhe. Mchengerwa amesema ni jukumu la watendaji wa ofisi yake kuzisaidia taasisi zote za umma nchini kuwa na mifumo thabiti na imara ya kiutendaji ili zitoe huduma bora kwa wananchi na kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.

 “Hakuna taifa lolote duniani lililoimarika kiuchumi au kupiga hatua kimaendeleo bila ya kuwa na taasisi imara kiutendaji ambazo zina uwezo wa kutoa maamuzi sahihi na bila kuingiliwa,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

 Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Mchengerwa, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ameahidi kuwa ofisi yake kupitia Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi na Idara ya Ukuzaji Maadili kwa kushirikiana na idara nyingine itahakikisha inazijengea uwezo Taasisi za Umma ili ziwe imara kiutendaji kama alivyoelekeza.

 Akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Mchengerwa kwa niaba ya wajumbe wa baraza, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bibi Hilda Kabissa amewataka watumishi wa ofisi hiyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa umma iliyopo ili kutekeleza kikamilifu maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Mchengerwa.

 Mkurugenzi Kabissa amewakumbusha watumishi wenzie kuwa waadilifu kwani watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni kioo cha utumishi wa umma, hivyo wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na watumishi wa taasisi nyingine za umma.

 Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wenye lengo la kupitia bajeti ya Mwaka wa Fedha 2021/2022, kujadili Mpango Kazi na Mtiririko wake wa fedha utahitimishwa kwa wajumbe wa baraza hilo kupata fursa ya kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Haydropower Project) na Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa kuuelezea umma faida za ujenzi wa miradi hiyo mikubwa ya kimkakati.

 

No comments: