KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI NA DAWA ZA KULEVYA IMEKUTANA NA KUJADILIANA NA ASASI ZA KIRAIA
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya ilipokutana na Asasi za Kiraia zinazoshirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa lengo la kujadili mikakati ya kupambana na dawa za kulevya katika ukumbi wa mikutano Hoteli ya Nashera, Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya Mhe. Fatma Taufiq (Mb.). Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya Mhe. Fatma Taufiq (Mb.) akieleza jambo wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya Wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika kikao hicho cha majadiliano kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya na Asasi za Kiraia kilichofanyika Hoteli ya Nashera Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi akieleza jambo wakati wa kikao hicho cha majadiliano kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya na Asasi za Kiraia kilichofanyika Hoteli ya Nashera Jijini Dodoma. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya Mhe. Fatma Taufiq (Mb.) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga (kushoto).
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akieleza jambo wakati wa kikao hicho. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya Mhe. Fatma Taufiq (Mb.). Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gerald Kusaya.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gerald Kusaya akieleza hatua ambazo zimekuwa zikichukiliwa na Mamla hiyo katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya wakati wa kikao hicho cha majadiliano kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya na Asasi za Kiraia kilichofanyika Hoteli ya Nashera Jijini Dodoma.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(SERA, URATIBU, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
************************************
Na: Mwandishi wetu, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya imekutana na Asasi za Kiraia zinazoshirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa lengo la kujadili athari za dawa za kulevya zinazochangia katika maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI, kuharibu nguvu kazi ya Taifa na mikakati ambayo imekuwa ikichukuliwa kuwasaidia waraibu wa dawa hizo.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Serikali imeendeela kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kisheria kwa kuwachukulia hatua wale wanaojihusisha na uingiza wa dawa za kulevya kwani zimekuwa zikileta madhara makubwa na kusababisha mzigo mkubwa kwa serikali.
Aliipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya chini ya Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo (DCEA), Gerald Kusaya kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi Nchini katika kuhakikisha vitendo hivyo vinadhibitiwa katika maeneo mbalimbali kwani madhara yake ni makubwa kwa watanzania kiafya, huduma za tiba kwa watanzania, kiuchumi kupitia biashara haramu za dawa za kulevya na mahusiano ya kidiplomasia.
“Kwa mara ya kwanza tangu tupate uhuru muda mfupi baada ya uteuzi wa Kamishana jenerali kufanyika ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa kumteua ilifanikiwa kukamata dawa za kulevya za mchanganyiko kilo 859.36 kwa mara moja na mpenyo uliotumika kuingiza siyo ule tuliozoea Dar es salaam, Bagamoyo na Tanga lakini kumbe tulikuwa na mipenyo mingine Mikoa ya Kusini,Lindi na Mtwara kwenye fukwe za bahari kama siyo umahiri na upambanaji wa mamalaka hii mzigo huu ungetuponyoka,”alisema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama aliongeza kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanasababisha magonjwa sugu kama UKIMWI,Homa ya Ini, TB na mengineyo na kupotea nguvu kazi ya Taifa kwani asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana akisema watumiaji wa dawa hizo kwa wingi ni vijana na kusisitiza mamlaka hiyo kuendelea kuungwa mkono serikali katika kudhibiti dawa za kulevya.
“Ni bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tazania lilifanya mabadiliko ya sheria ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kuweka zuio kubwa la uingizaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90 niwapongeze viongozi waliotangulia kama bunge msingeridhia kule tulikokuwa mliona kabisa mamlaka haikuwaweza kutekeleza lakini leo tumefika hapa ni kwa sababu yenu wabunge na kamati wakati wa mabadiliko hayo mlituagiza kutengeneza kanuni ,utendaji kazi wa mamlaka na halmashauri zetu na kamati za ukimwi zipate nafasi ya kupambana na dawa za kulevya huko ndipo walipo hawa wadau wote,”alisisitiza.
Hata hivyo alisema bado kuna changamoto ya unyanyapaa kwa wanaotumia au waliowahi kutumia dawa za kulevya wakaacha kwa hiyo hilo ndilo tatizo linalotakiwa kufanyiwa kazi kuona kwa namna gani unyanyapaa utamalizika na kuwaruhusu wengi wajitokeze wapate tiba na warudi wakawe raia wema kwani madhara ya dawa yanaenda kuharibu afya ya akili.
Mbali na hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Taufiq (Mb.) alipongeza wadau wote na kusema janga la dawa za kulevya ni kubwa sana licha ya afua mbalimbali hivyo ipo haja ya kuweka nguvu ya pamoja na kukutana mara kwa mara ili kuona namna nzuri ya kuishauri serikali.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi alibainisha kwamba janga hili linaleta shida katika nyanja ya diplomasia, afya na maendeleo ya vijana ambo ndiyo nguvu kazi ya taifa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inaeleza kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini.
“Tunaahidi kufanya utafiti pamoja na kwamba kazi zinafanyijka katika mamlaka za mikoa lakini naona kuna haja ya kuongeza nguvu tujue chimbuko,athari na viashiria vya uwepo wa dawa za kulevya na twende tukaangalie namna ya kuongeza rasilimali fedha za kuwasadia waraibu wa dawa za kulevya,”alifafanua Naibu Waziri Katambi.
Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gerald Kusaya alisema utafiti umekuwa ukifanyika kwa kushirikiana Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kubaini hali ilivyo na hatua zinazoweza kuchukuliwa huku akisema kuwa waraibu wa dawa za kulevya wanaohudumiwa katika nyumba za kuwapatia Unafuu (SOBER HOUSE) wamekuwa wakijengewa uwezo kiuchumi kwa kuanzisha miradi ili wajikwamue.
“Nimetembelea hizo nyumba na wana miradi inayowafanya wajishughulishe, wapo wanafuga kuku, bustani na wanafanya mazoezi siyo kwamba wamekaa tunataka wawe na shughuli za kufanya na tunashirikiana na mamlaka za Mikoa ili tuwatafutie maeneo watakayofanyia shughuli za kiuchuni na tunashirikiana na wadau wa Umoja wa Mataifa kama Global Fund na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia dawa za kulevya na makosa mengine,” alieleza Kamishna Jenerali.
Akiwasilisha mada mbele ya kamati hiyo Msimamizi Huduma za Afya kwa waraibu wa dawa za kulevya kutoka mkoa wa Arusha, Bi. Jesca Temu alisema pindi mwathirika anapofikishwa katika kituo huchukua taarifa zake za awali na kumfanyia vipimo kufahamua aina ya dawa aliyotumia ili kujua matibabu yatakayomsaidia na kurejea katika hali yake ya awali aendeele katika shughuli za kijamii.
Aidha Katibu Mtendaji kutoka Gift of Hope Foundation kutoka iliyopo mkoani Tanga, Bw. Saidi Bandawe alieleza kuwa taasisi hiyo toka mwaka 2016 hadi 2021 imetoa elimu kinga kwa zaidi ya wanafunzi 5,000 dhidi ya dawa za kulevya, kutoa huduma ya Sober House 217 huku wakiwafikia waraibu wa dawa za kulevya 2,604 na kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayowasaidia kuendesha maisha yao.
No comments: