TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KUFANIKISHA UPATIKANAJI WA KIBALI CHA KUINGIZA NYAMA NCHINI SAUDI ARABIA



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kukamilisha taratibu za msingi za upatikanaji wa kibali cha kuingiza nyama za mifugo nchini Saudi Arabia baada ya kibali hicho kusitishwa kwa miaka kumi na tisa.

Hayo yameelezwa na Mhe. Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Ali Jabir Mwadini leo tarehe 3 Septemba, 2021 Jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Kibiashara uliohusisha wawekezaji kutoka nchini Saudi Arabia na Wadau wa Biashara na Uwekezaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA ), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Kituo cha Uwekezaji Tanzania ( TIC) pamoja na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).

Akiongea baada ya kumalizaka kwa Mkutano huo Mhe. Balozi Mwadini amesema Tanzania imefanikiwa kupiga hatua kubwa kwa kuhakikisha zoezi la wataalam wa Mamlaka ya Chakula na Dawa kutoka nchini Saudi Arabia wamefika nchini kukagua machinjio zetu kwa ajili ya kutupatia kibali cha kuuza nyama za mifugo nchini humo.

“ Ni takribani miaka kumi na tisa toka kusitishwa kwa kibali cha kuingiza nyama nchini Saudi Arabia hivyo, baadhi ya taaratibu ilibidi zifatwe ili kukapata kibali hicho ambapo timu ya ukaguzi kutoka nchini Saud Arabia ilifika hapa mnamo tarehe 01 Agosti, 2021 ambao walitembelea Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na walipewa taarifa za Mamlaka ya Dawa (TMDA) ambapo kwa taarifa za awali zinasema walijilidhisha kuwa tunauwezo wa kupeleka bidhaa zenye ubora nchini Saudi Arabia ” Alisema Mhe. Balozi Mwadini

Mhe. Balozi Ali Jabir Mwadini aliendelea kufafanua kuwa hatua hiyo ni matokeo ya Mikutano ya Biashara kwa njia ya mtandao iliyoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) mwezi Disemba, 2020 hadi Februari, 2021 ambapo, katika mikutano hiyo kampuni mbalimbali kutoka nchini Saudi Arabia zilikuwa tayari kununua nyama za mifugo inayozalishawa hapa nchini hivyo waliitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha wanafanikisha uhakiki wa machinjio ya Ngo’mbe hapa nchini ili kujiridhisha kama yamefikia vigezo vya soko la Saudi Arabia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi. Latifa Khamis ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia kwa kuhakikisha zoezi la wataalam wa Mamlaka ya Chakula na Dawa kutoka nchini Saudi Arabia wamefika nchini na kukagua machinjio zetu kwa ajili ya kupata kibali cha kuuza nyama za mifugo nchini humo. 


 

No comments: