WAZIRI AWESO 'AMTUMBUA' MHANDISI WA MAJI KONGWA
Charles James, Michuzi TV
UKINIZINGUA Nakuzingua! Ni kauli ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ambayo amekua akiitoa kwa watendaji wa Wizara hiyo ambao wamekua hawana ufanisi kazini au wale wanaohujumu miradi ya maji nchini.
Kauli hiyo imemtokea puani Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma, Mhandisi Hubert Kijazi kutokana na kushindwa kusimamia mradi wa Maji wa Mkoka ambao ameutekeleza na kushindwa kutoa Maji yanayofaa kwa binadamu.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Waziri Aweso alipofanya katika Wilaya ya Kongwa kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kutatua kero za maji zinazowakabili wananchi wa Wilaya hiyo.
Meneja huyo wa RUWASA aliyetumbuliwa kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara ameshindwa kushauri juu ya mradi huo na kuisababishia Serikali hasara ya Sh Milioni 609 kwani Maji yanayotokana na mradi huo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Waziri Aweso alichukua uamuzi huo baada ya kufika na kujionea mradi huo lakini pia kupata malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya ladha ya maji hayo na alipoagiza kuchukuliwa vipimo vya maabara majibu yalionesha Maji hayo yana Chumvi nyingi na hayafai kwa matumizi ya kibinadamu.
" Hapa tumeongozana na Naibu Katibu Mkuu wetu ambaye ni mtaalamu amethibitisha kuwa Maji haya hayafai kwa matumizi ya kibinadamu, hivyo nimuagize Katibu Mkuu wetu Mhandisi Sanga kumchukulia hatua huyu mtaalamu ambaye ameshindwa kutumia utaalamu wake kutushauri kama Serikali.
Nimuagize pia Meneja wa RUWASA Mkoa aniandikie barua ya kujieleza kwanini tusiwafukuze kazi kwa sababu kama wao wapo na bado wanashindwa kuchukua hatua hadi Serikali inapata hasara kubwa hivi huku wananchi wetu wakiendelea kupata shida ya maji, niandikieni barua mnieleze kwanini tusiwafukuze kazi?," Amesema Waziri Aweso.
Aweso pia amewaagiza watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha hadi kufikia Jumatatu wawe wamepeleka vifaa vya uchimbaji wa kisima kingine chenye maji laini yanayofaa kwa matumizi ya binadamu huku akiwaomba radhi wananchi hao na kuwahakikishia kuwa changamoto hiyo ya Maji itaisha ndani ya muda mfupi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Selemani Serera amemshukuru Waziri Aweso kwa kufika Wilayani hapo na kusikiliza Changamani za wananchi pamoja na kuzitatua.
Amesema uwepo wa Maji ya uhakika Wilayani humo kutachangia ukuaji wa maendeleo kwa wananchi pamoja na kukua kwa uchumi wake.
Mkuu wa Wilaya Kongwa, Dk Selemani Serera akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na wananchi wa Kongwa.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Kongwa alipofika kukagua miradi ya maji Wilayani humo. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Kijiji Cha Ijaka Wilayani Kongwa alipofika kukagua mradi wa Maji na kutatua changamoto za maji kwa wananchi hao
No comments: