WATAALAM WAKUTANA DAR, WAZINDUA 'ELIMU UMEME FOUNDATION' KUEPUKA MAJANGA YANAYOTOKANA NA UMEME


Mkurugenzi Mkuu wa Geared Consulting Engineeers Ltd Mhandisi Warda Ester Mash'mark (katikati) akiendelea kusoma hotuba yake ya ufunguzi. (wa kwanza kulia ) ni Mkuu wa Masoko wa Taasisi hiyo Janolin Jonas, na (kushoto) ni wakili wa kujitegemea ambae pia mjumbe wa Taasisi hiyo Faith Kiwanga.
Mkurugenzi Mkuu wa Geared Consulting Engineeers Ltd Mhandisi Warda Ester Mash'mark (kulia) Akizungumza na akiwawageni mbalimbali na waandishi wa habari waofika kwenye uzinduzi huo. (Kushoto) ni Mjumbe wa Taasisi hiyo Wakili Faith Kiwanga.
INSP Isack Njombe kutoka Jeshi la Zimamoto Kinondoni Akizungumza mbele ya wajumbe mbalimbali waliohudhuria kwenye hafla hiyo Jijini Dar es Salaam.
Meneja Maendeleo ya Biashara Benki ya NBC Tawi la Mlimani City Eliezer Kabango akiasilisha mada maalum ya namna wadau wa umeme watakavyoweza kunufaika na huduma zao kwenye hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Elimu Umeme Foundation'  Jijini Dar es Salaam.
Wakili Asella Arcard kutoka Taasisi ya A & F Attorneys akiwasilisha mada wakati wa hafla hiyo.

Wadau mbalimbali waliohudhuria kwenye hafla hiyo wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mkurugenzi Warda Mash'mark.

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WATALAAM wa umeme nchini wamesema ni muda sahihi kuwekeza kwenye elimu juu ya misingi ya umeme katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na mikakati yake ya kuwekeza na kusambaza umeme mijini na vijijini.

Akizungumza mbele ya wadau wa nishati ya umeme wakati wa uzinduzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya 'Elimu Umeme Foundation' Mkurugenzi Mkuu wa Geared Consulting Engineeers Ltd Mhandisi Warda Ester Mash'mark amesema mfumo wa umeme kama ilivyo mifumo mingine inafuata viwango vya kitaifa na kimaifa, hata hivyo viwango hivyo vinabadilika, hivyo mitaala haibadiliki kuendana na viwango hivyo.

Ameongeza lengo kuu la taasisi hiyo ni kufundisha jamii matumizi sahihi na salama ya umeme ikiwemo miundombinu yake na pia kwa kushirikiana na Serikali kuboresha mitaala shuleni, taasisi za ufundi na vyuoni.Hivyo kupitia Elimu Umeme Foundation watashiriki kikamilifu utoaji elimu inayohusu masuala ya umeme,"amesema .

Amefafanua kwa kutoa mfano tangu mwaka 2004 rangi za nyaya za umeme zilifanyiwa mabadiliko, ambayo yalisababisha kubadilishwa ngazi ya kitaifa(TBS-2012).Hata hivyo kuna mkanganyiko kwasababu kuna rangi za zamani bado ziko sokoni.

Aidha amesema kwa upande wa matumizi ya umeme wateja wa umeme kama viwandani, majengo na wengine wengi kutokana na kukosa elimu juu ya viwango vya umeme, wamekuwa wakilipa gharama kubwa , hivyo bidhaa zinazozalishwa nchini hukosa ushindani sokoni kutokana na gharama ya uzalishaji.

"Hii imekuwa ikisababisha wadau wengi zikiwemo taasisi za Serikali na binafsi wakati mwingine kushindwa kulipa ankara 

na kupelekea kukatiwa umeme,hii yote inatokana na ukosefu wa elimu na hivyo sisi tumeamu kuja na Elimu Umeme Foundation kusaidia kutoa elimu,"amesema.

Amesisitiza kwamba Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kwenye uzalishaji na usambazaji umeme , hivyo kasi hiyo iandane na wananchi kuujua umeme na kuchukua tahadhari zote ili kuepuka majanga yakiwemo vifo.

"Tunaiomba Serikali na taasisi binafsi zituunge mkono kwa hali na mali ili uwekezaji kwenye umeme uende sambamba na elimu,"amesema Mhandisi Mash'mark.

Amesisitiza kazi ya kutoa elimu ni ngumu kwani matatizo kwenye mifumo ya umeme ni mengi lakini wameanza kutekeleza japo kwa uchache na kikubwa zaidi kinachokwamisha ni gharama za uendeshaji na ushirikiano duni kutoka taasisi za kiserikali.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zima Moto Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es Salaam Inspekta Isack Njombe amesema taasisi hiyo kwa namna moja au nyingine wanalisaidia jeshi la zima moto katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya umeme.

Amefafanua kuwa majanga mengi ya moto yanatokana na hitilafu za umeme ambazo nyingine zinatokana na kukosekana kwa elimu sahihi ya matumizi ya umeme."Jeshi la Zima Moto tumekuwa tukitoa elimu inayohusu matumizi sahihi ya umeme ili kuepuka majanga, hivyo wenzetu hawa wanatusaidia."

No comments: