Zantel yajizatiti kuboresha mtandao wa 4G visiwani Zanzibar
· Ni kupitia kampeni yake ya Pasua Anga Ki Zantel 4G inayotoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mtandao wa 4G
Pemba.Mei 19, 2021.Kampuni ya Mawasiliano ya Zantel, imeeleza mpango wake wa kueneza na kuboresha zaidi mtandao wa 4G katika kila kona ya visiwa vya Zanzibar ili kutoa fursa kwa watumiaji kunufaika na mtandao huo hasa kujiendeleza na shughuli za kiuchumi mtandaoni.
Mkakati huo ni sehemu ya kampeni yake mpya ijulikanayo kama ‘Pasua Anga Ki Zantel 4G’ yenye lengo la kutoa elimu juu ya matumizi yenye tija ya mtandao wa 4G hususan kujiendeleza kiuchumi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika viwanja vya Gombani Kongwe visiwani Pemba, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Zantel, Bi.Aneth Muga alisema lengo kubwa ni kuhakikisha wateja wananufaika zaidi na matumizi ya intaneti mbali na matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Leo tunafuraha kuwajulisha wateja wetu kuwa tumerudi tena na kampeni yetu hii mahsusi ili kuendelea kutoa elimu kwa wateja wetu juu ya manufaa mbalimbali yatokanayo na mtandao ulioboreshwa wa Zantel 4G,” alisema Muga.
Aliongeza kuwa Zantel inaendelea kuboresha mtandao ili kwenda na kasi ya ulimwengu kidigitali ikiwamo kufanya uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwamo minara mipya ya simu hasa kwenye maeneo ya vijijini ili kuwafikia watu wengi zaidi.
“Nia yetu ni kuendelea kuboresha mtandao wetu ili mawasiliano yapatikane Zanzibar yote kwa kasi ya 4G na kumuwezesha mtumiaji kupata mawasiliano bora na ya haraka,” alisema Muga.
Ni wazi kuwa kupitia simu ya mkononi tu unaweza kufanya mambo mengi sana kwa haraka na urahisi zaidi. Mfano, kukata tiketi za safari mbali mbali kama boti, kununua na kuuza bidhaa mbali popote ulimwenguni kwa muda mfupi,kupata elimu, kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki.
“Kwanza kabisa, kupitia intaneti ya 4G mteja wetu anapata spidi ya kasi ambayo inamuwezesha kufanya shughuli zake mtandaoni haraka na kwa urahisi zaidi. Hii inamfanya mtumiaji kupata taarifa kwa haraka zaidi tofauti na yule anayetumia 3G,” alisema
Kwa upande wake, Mkuu wa Mauzo na Usambazaji wa Zantel Kanda ya Pemba, Said Masoud Ali alisema mpango ni kuhakikisha kila mtu anafikiwa na mtandao wa 4G ikiwamo kuwawezesha watu kupata simu za bei nafuu.
“Tumeleta simu ambazo zina uwezo wa 4G na tunaziuza kwa bei nafuu ambapo tunatoa punguzo hadi asilimia 5 pamoja na GB 24 bure mwaka mzima, hii inasaidia kila mtu kupata mtandao wetu wa 4G,” alisema Ali.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Zantel, Bi.Aneth Muga(katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mauzo na Usambazaji wa Zantel,Emmanuel Swai (kushoto) na Mkuu wa Mauzo na Usambazaji wa Zantel Kanda ya Pemba, Said Masoud Ali wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Pasua Anga Ki Zantel 4G uliofanyika katika viwanja vya Gombani Kongwe visiwani Pemba.Kampeni hiyo imelenga kutoa elimu juu ya umuhimu wa mtandao wa 4G kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi
No comments: