Serikali yaombwa kuweka utaratibu wa kuwatambua watu wanaookota makopo

Mpigapicha wa kujitegemea Imani Nsamile akielezea kwa waandishi wa habari namna picha ya inavyoweza kufikisha ujumbe wa mazingira kwa watu wengi na wakaweza kujifunza wakati wa wiki ya ubunifu inayoendelea katika kumbi za LAPF, kijitonyama Dar es Salaam.
Katibu wa masuala ya Uchumi wa Ubalozi wa Uholanzi, Mathijs van Eeuwen mwenye suti akijadiliana jambo juu ya mabadiriko ya tabia nchi wakati wa wiki ya ubunifu inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu.
SERIKALI imeaswa kuweka utaratibu wa kuwatambua watu wanaookota makopo nchini na kuwaingiza kwenye ajira rasmi ili kuwapa motisha watu wengi zaidi kufanya hiyo kazi ili kuboresha kazi zao katika kuendelea kuimarisha sekta ya mazingira

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Nipe Fagio Ana Rocha ameyasema hayo leo Mei 19, 2021 jijinj Dar es Salaam wakati akizungumzia namna mabadiliko ya tabia nchi na mazingira yanavyoendelea kuiathiri nchi yetu kwenye maadhimisho ya wiki ya ubunifu yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema, mbali na serikali , Taasisi binafsi na makampuni mbali mbali yanaweza kufanya hivyo kwa kuwapa nafasi ya kuboresha kazi zao, maisha yao na kuwapa heshima sababu ni watu muhimu sana katika sekta ya mazingira.

"Hawa waokota makopo ni watu wa muhimu sana katika nchi yetu kwa ulinzi wa mazingira, kwa sababu wao wanatembea wanachukua machupa ya plastiki na vitu vingine ambavyo wanavipeleka kiwandani vikitengenezwa vinaweza kutumika tena wakati kama visingeokotwa vingeweza kukaa kwenye mazingira kwa miaka mingi." Amesema Rocha.

Ni vema pia jamii ikawapa heshima, nafasi na kuwaonyesha upendo kwa sababu wengi wa wanaofanya kazi hiyo ya kuokota makopo wanaishi maisha magumu na jamii inawaangalia bila kuwapa heshima huku kazi wanayoifanya ikiwa ni ya muhimu na kusaidia sekta ya afya na mazingira.

"Sisi kwenye mfumo wetu wa taka sifuri tunawaingiza kwenye mfumo ambapo wanaingia kabisa na kuanza kuhudumia nyumba kwa kuokota taka na kuzipeleka kwenye eneo sahihi." Amesema Rocha.

Aidha, ubalozi wa Ufalme wa Uholanzi, umesema kazi za wasanii zinazoonyeshwa kwa njia ya picha na video zinaweza kutumiwa kuonyesha uelewa juu ya shida za hali ya hewa ulimwenguni kutokana na mabadiriko ya tabia nchi.

Katibu wa Kwanza Masuala ya Uchumi wa Ubalozi huo, Mathijs van Eeuwen amesema, walifanya maonyesho ya picha 21 na video kutoka Tanzania na tatu zilichaguliwa kwa ujumbe wao wenye athari katika mazingira.

"Kuona kwa macho kuna tabia ya ushawishi, picha huzungumza mengi juu ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa." Amesema.

Kwa upande wake, mpiga picha kutoka Tanzania Imani Nsamile amesema mwaka 2016 alipiga picha moja mkoani Singida katika kijiji cha Mkalama ambapo picha ilionyesha namna wananchi wa kijiji huu hicho walivyokuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji.

Amesema picha hiyo ilionyesha ujumbe tofauti ikiwa ni pamoja na jinsi watoto walivyokuwa wakipaswa kukosa kwenda shule ili kwenda kutafuta maji na hivyo kupoteza muda wakuandaa maisha yao ya baadaye na wakati huo huo jinsi wanawake walikuwa wakitumia wakati wao mwingi kutafuta maji na hawafanyi shughuli zingine za maendeleo kwa familia.

"Picha hiyo pia ilionyesha jinsi mifugo inavyokuwa imekonda kutokana na ukosefu wa lishe bora kufuatia uhaba wa maji," amesema.

Alisema kufuatia picha hiyo, watunga sera na umma pia walifahamishwa jinsi mabadiliko ya hali ya hewa yanawaathiri na kuchukua hatua.

Katika hatua nyingine, mpiga picha kutoka Uholanzi, Kader Van Lohuizen amesema kufuatia athari mbaya kwa mazingira ambayo amekuwa akitumia picha kuonyesha jinsi kupanda kwa joto kumekuwa kukiathiri sehemu zingine za ulimwengu.

Mkataba wa Paris unasema kwamba joto halipaswi kuongezeka kwa zaidi ya nyuzi 2 duniani. "Ikiwa halijoto haitashuka katika maeneo ya pwani, itakuwa mbaya," alisema.

Akielezea alisema, huko Indonesia maji yalikuwa yakiongezeka kwa kasi ya sentimita 20 hadi 30 kila mwaka na kuufanya mji katika ukingo wa kuporomoka, na kuilazimisha serikali kuhamisha mji mkuu wote.

Huko Bangladesh alisema kuna dhoruba nyingi na vimbunga, na maji ya bahari hayapunguki hivyo huathiri ardhi ambayo hutumiwa kwa kilimo na kuchafua maji ya kunywa.

No comments: