TSC YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

 
 Na Veronica Simba - TSC
 
Wafanyakazi wanawake wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Makao Makuu Dodoma, wameadhimisha siku ya wanawake duniani kwa ufanisi.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo, Machi 8, 2021 jijini Dodoma, Wafanyakazi hao wameshiriki katika maandamano yaliyoshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, yaliyoanzia Uwanja wa Jamhuri hadi katika Uwanja wa ‘Nyerere Square.’

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wanawake wa TSC, Mwenyekiti wao, Catherine Kamili ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwathamini wanawake na kuwapatia nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali nchini.

Aidha, amewataka wanawake wote nchini, hususani watumishi wa TSC, kuendelea kuchapa kazi kwa weledi na kujituma katika kuhakikisha, wanakuwa sehemu ya waleta maendeleo ya jamii na Taifa.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kitaifa, mwaka huu ni “Wanawake katika Uongozi, Chachu kufikia Dunia yenye Usawa.”

Wafanyakazi wanawake wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Makao Makuu Dodoma, wakishiriki katika maandamano wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 2021.
 Baadhi ya wafanyakazi wanawake wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), wakiungana na wenzao kutoka Taasisi mbalimbali kucheza, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa ‘Nyerere Square’ jijini Dodoma, Machi 8, 2021.

No comments: