NIC, TPB WAKUBALIANO KUTOA HUDUMA ZA BIMA KWA PAMOJA KWA WATEJA WAO
SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC,) na Benki ya TPB wameingia makubaliano ya kutoa huduma za Bima kwa pamoja kwa wateja wao ili kufikia lengo la sekta ya bima na kuhakikisha asilimia 50 ya watanzania wanafikiwa na huduma za bima ifikapo mwaka 2028.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mkoani Dar es Salaam ,Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TPB Bank, Sabasaba Moshingi amesema, huduma za bima bado zipo chini lakini kupitia ushirikiano huo na watapiga hatua katika kutoa huduma za bima zinazohitajika kwa kiasi kikubwa na Watanzania.
"Kwa taarifa nilizozipata lengo la sekta ya bima ni kuhakikisha asilimia 50 ya watanzania wanafikiwa na huduma za bima ifikapo mwaka 2028 na kwetu tumedhamiria kuhakikisha watanzania wanapata huduma za kifedha ikiwemo kutoa fedha na kufungua akaunti na kupata huduma za mikopo...
*Lakini suala la bima ni muhimu zaidi niwapongeze NIC kwa kutuamini na kutupa nafasi, niwahakikishie kuwa sisi tupo kibiashara na tumefarijika sana na tutadumisha mahusiano haya katika kuendeleza soko la bima nchini,"amesema.
Aidha amesema benki hiyo italipa ada ya awali kwa wateja wa NIC kupitia mkopo wenye riba wenye pamoja na kuendelea kubuni bidhaa za bima za maisha pamoja na huduma nyingine za bima kwa malengo ya kuwasaidia watanzania katika kupata huduma za bima na fedha.
"Tunategemea kuunganisha mifumo ya usajili wa bima yaani wa TPB na NIC na kuendelea na harakati za pamoja za kukuza uelewa wa bima kwa wananchi kote nchini na niwaombe wananchi na wateja wote wa TBP kutembelea matawi yetu yaliyopo kote nchini ili waweze kupata huduma za bima bora zaidi kutoka NIC,"amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC,) Dkt. Elirehema Doriye amesema, NIC inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 hivyo watanzania hawana budi kufurahia makubaliano hayo na TPB ambayo pia inamilikiwa na Serikali na wanahisa wachache.
"Tunawafikishia huduma kwa ukaribu zaidi kupitia matawi ya NIC na TPB kote nchini, tumezogeza huduma karibu ili tuweze kuwahudumia na kuwasilikiza wananchi kwa ukaribu zaidi." Amesema.
Pia amesema, benki ya TPB ina wataalamu wa bima kwenye kila tawi nchini na hiyo ni katika kutengeneza bidhaa za bima zinazojibu maswali ya kibima yenye uhitaji zaidi kwa Watanzania.
Amesema kupitia TBP, wanawawezesha Watanzania kupata huduma za kibima bila kuwa na fedha mkononi bali kwa kukopa kupitia TBP kupitia makubaliao yao kwa bei nafuu na kupata huduma zote muhimu za kibima.
"Makubaliano haya yana mtazamo chanya kwa watanzania na ndoto za Rais Magufuli kwa watanzania tunaamini zitafikiwa kupitia hili na nimuhakikishie Sabasaba tutakuwa pamoja katika hili na kufanikisha kutimiza ndoto za watanzania wengi,"amesema.
No comments: