Wakulima wa chai Njombe waliotaka kugoma kuchuma majani wapigwa 'stop'

Na Amiri Kilagalila,Njombe
MKUU wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya ameagiza wamiliki wa viwanda vya chai vya Lupembe estate na kampuni ya DL kufika ofisini kwake jumatatu wakiwa na taarifa za utekelezaji wa maelekezo waliyopewa kuhusiana na malipo ya wakulima na wasafirishaji wa chai.

Agizo hilo amelitoa leo katika kikao na waandishi wa habari ambacho kimefanyika ofisini kwake hapa mkoani Njombe.

Amesema kwa kipindi kirefu kumekuwa na mgogoro wa wakulima wa chai kutolipwa fedha zao na wamiliki wa viwanda vya kuchakata chai.

Amesema wakulima na wasafirishaji walikuwa wanadai fedha zao kuanzia mwezi wa kumi mwaka jana hadi januari mwaka huu ambapo fedha wanazodai ni shilingi milioni 996.

"Jana nilifanya kikao na viongozi na wakulima wa chai kule Lupembe katika kikao hicho ilibainika kuwa wamiliki hawa bado hawajalipa fedha za wakulima na fedha za wasafirishaji kama nilivyoelekeza kwenye barua yangu" amesema Rubirya.

Aidha amesisitiza kuwa zoezi la kusitisha uchumaji wa chai halikubaliki kwasababu viwanda vinahitaji malighafi licha ya kuwa wakulima nao wanahitaji fedha zao kwa ajili ya kuendesha maisha yao na familia zao.

Amesema pia siku hiyo atakutana na mbunge wa jimbo la Lupembe na madiwani ambapo atatoa maelekezo na msimamo wa serikali.juu ya suala hilo.

"Ni lazima kuvuna chai kwasababu inahitajika viwandani kitendo chochote cha kuendelea kusitisha uvunaji wa chai kinatafsiriwa kama ni uhujumu uchumi" amesema Rubirya.

No comments: