WANAWAKE NBAA WASHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Tarehe 8 Machi ya kila mwaka ni Siku ya wanawake duniani, ambapo siku hii inataka kukumbushia na kutafakari juu ya matokeo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi waliyofikia wanawake na msimamo wao imara katika ngazi ya kijamii kwa ujumla.
Katika kuadhimisha siku hiyo Wanawake wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania(NBAA) wameshiriki maadhimisho hayo yaliyofanyika leo Mkoani Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Wanawake katika Uongozi, chachu kufikia Dunia yenye usawa” Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Wanawake wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania(NBAA, Irene Mutagaywa amewataka wanafunzi walioko mashuleni kujikita katika kutengeneza ndoto zao kwa kusoma kwa bidii ili kuwa sehemu ya wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali hapo baadaye.Pia amesema mafanikio yoyote yanayoonekana nchini na duniani kote kwa kiasi kikubwa pia yamechagizwa na uwepo wa wanawake huku pia akimpongeza Rais Dk John Magufuli kwa kuendelea kuwaamini wanawake katika nafasi mbalimbali za kiuongozi kwenye Serikali yake.
Siku ya wanawake duniani ilianza kutokana na jitihada za wanawake 15,000 mwaka 1908 walipoandamana mjini New York Marekani wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura. Kilikuwa ni chama cha kisoshalisti cha Amerika kilichotangaza kuwa ni siku ya kwanza ya kitaifa ya wanawake, mwaka mmoja baadaye. Wazo la kuwa siku ya kimataifa lilianzishwa na mwanamke kwa jina la Clara Zetkin. Yeye alipendekeza wazo hilo mwaka 1910 katika mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi wanawake huko Copenhagen Denmark.
No comments: