Mbunge wa Ludewa akabidhi mbegu za Mihogo kuimarisha usalama wa chakula tarafa za Mwambao na Masasi
Na Amiri Kilagalila,Njombe
Wananchi wa tarafa za Mwambao na Masasi,wilayani Ludewa mkoani Njombe wanatarajia kunufaika na mbegu ya kisasa ya zao la mhogo iliyotolewa na ofisi ya mbunge wa jimbo hilo ili kuendelea kuimarisha upatikanaji na usalama wa chakula.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mbegu hizo,katibu wa mbunge wa jimbo la Ludewa Alphonce Mwapinga, amesema zoezi la ugawaji wa mbegu limeanza tarehe 12 mwezi wa Pili mara baada ya kupokea kutoka mkoani Mara huku wanufaika wakiwa ni wananchi wa tarafa za Mwambao na Masasi kupitia vikundi vya wakulima waliopo katika kata ndani ya tarafa hizo.
“Mbegu hii tunaigawa kwa kutumia kwenye vikundi na kila kata ina kikundi kimoja ambacho kitalima na tutatumia kama shamba darasa kwa lengo la kuzalisha mbegu kwasababu Mh,Mbunge ana mpango wa kuona kila eneo linazalisha mhogo kwa wingi kwasababu wilaya yetu ya Ludewa ina mazao ya kimkakati ambayo ni kahawa,pareto,parachichi,korosho na kwenye mazao ya chakula tumeweka zao la muhogo”alisema Mwapinga
Aliongeza kuwa malengo ni kuzifika kata zote ambapo mpaka sasa vikundi nane viliyopo vitakabidhiwa mbegu hiyo.
“Lengo la kuyafanya haya yote ni kwasababu wilaya yetu ni ya kilimo na watu wake wanapenda kazi na changamoto za chakula zitakapojitokeza sisi tuwe na zao la kujihami kwa maana hiyo tunataka kujiimarishia usalama wa chakula”alisema tena Alphonce Mwapinga
Lukas Mwakalebela ni afisa kilimo wilayani humo,amesema mbegu waliyoipokea inaitwa Mkombozi ambayo uzalishaji wake uko vizuri na inafaa kwa kula mhogo ukiwa mbichi pamoja na kutumika kwa matumizi ya unga na hata kupika mihogo.
“Kama alivyosema Mh,Mbunge katika maelekezo yake ni kwa ajili ya uzalishaji uongezeke katika maeneo hayo lakini pia usalama wa chakula anagalau kwa kila kaya”alisema Lukas Mwakalebela
Akizungumza kwa niaba ya wanachi wa tarafa ya Mwambao,afisa tarafa wa tarafa hiyo Bwana Linus Malama,ameahidi kuwa namashamba darasa ya kutosha kwa ajili ya zao hilo vile vile amesema kwa kuwa katika tarafa ya Mwambao zao hilo hutumika kwa ajili ya chakula na biashara wanaamini mbegu hiyo itakuwa ni mkombozi kwao.
Venati Kayombo ni afisa mtendaji wa kata ya Lupingu na Venanti Lupagalo ni afisa mtendaji wa kata ya Lifuma wamemshukuru Mbunge kwa msaada wa mbegu kwa kuwa katika kata zao mbegu hiyo ni muhimu na wanaamini itakwenda kumfikia kila mwananchi.
“Ninaamini mbegu imefika muda mwafaka na kwa kuwa tunakwenda kuzalisha sasa basi itakapofika mwezi wa 12 mbegu hii itakuwa imemfikia kila mkulima anayelima Mhogo”alisema Venanti Lupagalo
No comments: