WFP, TRC WAKABIDHIANA MABEHEWA 40, DOLA LAKI SITA ZATUMIKA KUFANYA MATENGENEZO


Naibu Waziri wa UJenzi na Uchukuzi Mhandisi. Godfrey Kasekenya (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa safari za mabehewa 40 yalikabidhiwa leo na Shirika la Mpango wa Taifa Duniani (WFP,) kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kushoto kwake ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TRC John Kondoro na kulia kwake ni Mkurugenzi na Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Sarah  Gordon.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi. Godfrey Kasekenya akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa WFP na TRC mara baada ya hafla ya makabidhiano ya mabehewa hayo, leo jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi. Godfrey Kasekenya (aliyeshika bendera) akiruhusu mabehewa hayo kuelekea bandarini kupakia mizigo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi. Godfrey Kasekenya akifurahi na uongozi wa WFP NA TRC mara baada ya kupokea mabehewa 40 ambayo yameanza kufanya kazi punde mara baada ya kupokelewa.


*Mhandisi Kasekenya aitaka TRC kutoa huduma bora kwa wateja na kukusanya mapato kielektroniki

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP,) kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania wamemekabidhi mabehewa 40 ya mizigo yaliyotengenezwa kwa gharama ya dola za kimarekani laki sita zilizotolewa na WFP kwa Shirika la reli Tanzania (TRC,) ili kuongeza kasi ya utendaji kazi wa Shirika hilo na kuongeza mtandao mpana zaidi wa usafirishaji wa mizigo nje ya nchi na kuweza kuongeza pato la Taifa.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema, WFP wamekuwa washirika wazuri katika matumizi ya huduma za reli, wamekuwa wakitumia usafiri wa reli katika usafirishaji wa chakula kwa nchi zenye wakimbizi na kuokoa asilimia 40 ya fedha ya bidhaa zinazosafirishwa.

Mhandisi Kasekenya amesema, uimarikaji wa bandari ya Dar es Salaam uhitaji wa mabehewa umekuwa ukihitajika zaidi na WFP wamefungua njia na kuwataka wadau wengine zikiwemo Taasisi za Fedha na Mabenki kuunga juhudi hizo.

Aidha ameipongeza TRC kuwa kusimamia vyema ukarabati wa mabehewa hayo yaliyotengenezwa na watanzania bila kuomba msaada wa utaalam kwa asilimia miamoja na kuwataka kukarabati mabehewa yaliyopangwa kukarabatiwa kwa mwaka huu wa fedha.

"Serikali ipo imara, na TRC mnafanya vizuri, tunashukuru WFP kwa kukamilisha hili na tunawakaribisha wadau wengi zaidi, Niwaombe TRC mfanye kazi kwa kuwajali wateja wakati wa kutoa huduma na mkusanye mapato kwa njia ya kielektroniki ili kuweza kufikia malengo." Amesema Kasekenya.

Akizungumza katika makabidhiano hayo Mkurugenzi na Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson amesema, WFP imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali katika kuimarisha uwezo wa mnyororo wa ugavi wa Taifa katika sekta ya usafirishaji.

"Mwaka 2019 TRC na WFP zilitiliana saini makubaliao (MoU,) kwamba iwekeze dola za kimarekani laki sita ili kukarabati mabehewa 40  kwa kuboresha sekta hiyo katika kuimarisha uwezo wa ushoroba uliofunguliwa upya na kuunganisha usafiri wa reli hadi ziwa Victoria hadi Uganda na kupitia modeli hii Tanzania hunufaika na kunufaisha pia nchi za Uganda na Sudani Kusini." Amesema.

Pia amesema WFP hutumia reli kama sehemu ya mfumo wa Uchukuzi ili kusambaza bidhaa za chakula katika utekelezaji wa majukumu yake.

Sarah amesema, Tanzania imepakana na nchi nane na sita kati yake hazina bandari na WFP inaendealea kuisaidia Tanzania ili kufungua zaidi lango la usafirishaji na fursa za uwekezaji na biashara katika ukanda wa Afrika.

Vilevile amesema, tangu mwaka 2018 hadi 2020 WFP imenunua bidhaa za chakula tani 262,000 na kuliingizia Taifa pato la jumla ya dola za kimarekani milioni 160.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi MkuuShirika la Reli  (TRC) Masanja Kadogosa uwekezaji katika sekta hiyo umeendela kukua siku hadi siku na Serikali imekuwa ikiunga mkono jitihada zao na tayari imewekeza Trilioni kumi katika sekta hiyo.

Kadogosa amesema tayari Serikali imetoa fedha za kukarabati mabehewa 200 na kuwaomba wadau na washirika mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo ili kujenga uchumi wa Taifa.

No comments: