KESI YA MADAI KAMPUNI YA TAN COMMUNICATION YAHAIRISHWA
Na Woinde Shizza, Michuzi Tv -Arusha
MAHAKAMA kuu masijala Ndogo ya kazi Kanda ya Arusha leo imeahirisha kesi ya madai dhidi ya kampuni ya Tan communication inayomiliki kituo cha habari cha Radio Five na waliokuwa wafanyakazi Saba wa radio hiyo wanaodai zaidi ya sh, milioni 31.9 baada ya kuachishwa kazi kinyume na utaratibu.
Wafanyakazi hao wakiongozwa na Geoffrey Steven walifungua kesi ya madai nambari 151 ya mwaka 2020 baada kutoridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama ya usuluhishi (CMA) iliyompa ushindi mdaiwa.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Naibu Msajili wa mahakama, Ruth Masamu ilikuja katika mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa ambapo upande wa walalamikaji wakiongozwa na wakili Heri Makando walikuja kuiomba mahakama hiyo itoe idhini ya kukamatwa Mali za mdaiwa ambaye ni Tan Communication na kupigwa mnada ili kufidia malipo ya wafanyakazi hao.
Hata hivyo wakili wa upande wa mdaiwa, Andrew Maganga ameiambia mahakama hiyo kwamba amewasilisha notisi mahakama kuu ya rufaa inayohusu ku kupinga hukumu iliyotolewa na jaji Johannes Masara , June 16 ,2020 iliyowapa ushindi wadaiwa.
Naibu msajili wa mahakama hiyo, Ruth Masamu baada ya kupokea maombi hayo yaliyoambatana na notisi hiyo aliahirisha shauri hilo hadi Machi 16 mwaka huu.
Akiongea mahakamani hapo kwa niaba ya wenzake Geoffrey Steven alisema kimsingi wamepokea kusudio la rufaa hiyo na hivyo wanasubiri tarehe ya kusikiliza kwa shauri hilo
Hata hivyo ameongeza kuwa leo walikuja mahakani hapo kwa ajili ya kuiomba mahakama hiyo iweze kutoa idhini ya kukamatwa kwa mali za mdaiwa ambazo ni Jengo la kituo Cha Radio five, lililopo Njiro ploti namba 153 na 154 block J , Jenereta,vifaa vya studio na vifaa vya kurushia matangazo.
Wadai wengine katika shauri hilo ni Monica Nangu, Gloria Kaaya, Godluck Kisanga, Godfrey Thomas, Akidai kilango na Josephzat Nyamkinda.
No comments: