HIVI NDIVYO RAIS MAGUFULI ANAVYOWAELEZEA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, MHANDISI KIJAZI


*Asema wameondoka duniani wakiwa mashujaa, wamefanya kazi kubwa

Na Said Mwishehe,Michuzi TV.


RAIS Dk.John Magufuli amesema aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi John Kijazi wameondoka duniani wakiwa mashujaa kwa yale ambayo wameyafanya kwa ajili ya Watanzania.

Akizungumza mbele ya waombolezaji wakati wa kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi leo Februari 19,2021 jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amewazungumzia viongozi hao kila mmoja kwa nafasi yake na mchango wake kwa Taifa la Tanzania.

Akimzungumzia Maalim Seif , Rais Magufuli amesema jana katika mazishi ya Maalim Seif yeye hakwenda lakini alimtuma Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan amuwakilishe."Niseme tu Maalim Seif alikuwa kiongozi wa tofauti sana.

"Mwaka 2015 nilipoingia kuwa Rais na baada ya uchaguzi wa Zanzibar kufanyika ule wa marudio Maalim Seif aliniandikia barua ya kutaka kuja kuniona. Lakini nilisita, baadae aliandika barua ya pili nikawa kimya."Akaandika barua ya tatu, kila nilipokuwa nikiomba ushauri Zanzibar nilikuwa naambiwa nimuache kwanza.Siku moja nilimua kumuita Ikulu, katika mazungumzo yetu niligundua kumbe ni mtu wa tofauti sana.

 "Alielezea kuwa hakushiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio mwaka 2015 lakini Zanzibar itakuwa salama, hakutawa na vurugu, hatahamasisha vurugu, na kweli kauli yake ameithibitisha kwa vitendo,hata  ulipotokea uchaguzi mkuu wingine  alishiriki kwenye Serikali ya Muungano.Alikuja Chato, alinipa historia nzuri akiwa CCM na jinsi alivyoshiriki kuhamasisha wananchi kuipenda TANU.
"Maalim  Seif amemaliza salama na dhamira yake ya kujenga amani na umoja kwa Wazanzibar .Tutaendelea kuenzi yale yote yaliyofanywa na Maalim Seif katika kujenga umoja

KUHUSU MHANDISI KIJAZI
Rais Dk.Magufuli akimuelezea Mhandisi Kijazi amesema ana historia naye ndefu kidogo, baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 1995, alichaguliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ujenzi.

Amesema baada ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo aliamua kufanya ziara ya kutembelea maeneo mengi ya nchi na kukutana na wahandisi wa mikoa."Nilipotembelea Dodoma nilikuta barabara zote zinapitika.
"Licha ya kuwa za vumbi na nikamuuliza Kijazi kwanini barabara zako nzuri kuliko za wengine...akasema yeye anachokifanya kila senti inayotengwa kwenye barabara inatumika kikamilifu.
"Alinionesha fedha ambazo alikuwa anapelewa Dodoma zilikuwa ndogo kulinganisha na wengine, hivyo niporudi wizarani nilitoa ushauri kwa Waziri wangu Anna Abdallah, nikamuomba tumpromoti ili awe anafanya matengenezo ya barabara zote za Tanzania, hivyo akateuliwa na kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya matengezo ya barabar zote nchini,"amesema Rais Magufuli.


Ameongeza mwaka 2000 baada ya Uchaguzi Mkuu, yeye(Dk.Magufuli) aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na baada ya uteuzi huo aliamua kwenda Ikulu kumuomba Mzee Mkapa(aliyekuwa Rais wakati huo) ili Mhandisi Kijazi awe Katibu Mkuu katika Wizara hiyo."Nilikuwa nafanya makosa lakini nilijilipua, Mzee Mkapa alinishangaa na hakunijibu kitu alinyamaza lakini mwaka 2001, Mhandisi Kijazi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu, barabara nyingi zilitengenezwa akiwa katika nafasi hiyo.

"Mwaka 2005 nilienda Wizara nyingine, na Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimuona Mhandisi Kijazi kuwa bado anafaa akamuamini kwa kumpa nafasi na amefanya kazi katik sehemu nyingi.

"Alipokuwa India amefanya kazi kubwa sana , sote tunafahamu na alisababisha hata Waziri Mkuu wa India wakati huo kutembelea Tanzania, alifanya kazi za kizalendo.Nilipoteuliwa kuwa Rais nilitafuta nani wa kunisaidia kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, nikamuona Kijazi , hivyo nilimrudisha nchini, makatibu wakuu na watendaji wengine wataamini sikufanya makosa, hakuwa na makuu, hakujikweza,"amesema.

Ameongeza kuwa Balozi Kijazi alikuwa mnyenyekevu sana, hata alipotaka kumtumbua mtu alimwambia asubiri angalau kwa siku mbili au tatu."Kuna watu wako hapa wamebakia kwenye nafasi zao kwasababu ya Mhandisi Kijazi, 

"Wakati wa kuchambua miswaada iliyokuwa ikiletwa na makatibu wakuu alikuwa anaichambua vizuri , baraza la mawaziri tulikuwa hatupati shida, alizaliwa mwaka 1956 lakini mpaka leo amebakia kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

"Kwangu ni mkubwa kwa kuzaliwa, alitakiwa awe amestaafu lakini wakati ulipofika niliomuongeza miaka miwili ili nitafute mtu mwingine lakini miaka miwili ilipofika nikaona bado anatakiwa kuendelea tena nikawa namuongeza miaka miwili miwili lakini sikutapa wa kuwa kwenye nafasi yake,"amesema Rais Magufuli.

Amefafanua pamoja na majukumu yake, Mhandisi Kijazi alikuwa hakosi kwenda Kanisani, aliwatumikia watu wote kwa sawa."Ndugu zangu tumepata pengo lakini yote haya ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Baloz Kijazi ametanguliwa zamu yetu sisi bado, tujiandae na wakati wetu utakapofika." 

No comments: