Wagonjwa 159 wana matatizo ya afya ya akili wilayani Ludewa
Na Amiri Kilagalila,Njombe
Wananchi 159 wilayani Ludewa mkoani Njombe,wamebainika na kutibiwa matatizo ya afya ya akili kuanzia mwaka 2018 huku wengi wao wakifanikiwa kupata uponyaji na wengine wakiendelea na matibabu.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Dkt,Stanley Mlay amemueleza mwandishi wetu kuwa matatizo ya afya ya akili ni miongoni mwa magonjwa yanayotolewa matibabu katika halmashauri hiyo na mpaka sasa wameweza kuhudumia wagonjwa wasiopungua 159 kwa takwimu za kuanzia mwaka 2018.
Amesema ugonjwa wa kifafa ni moja ya tatizo kubwa linalochangia matatizo ya afya ya akili wilayani humo kwa kuwa na wagonjwa 115,Sailiosisi wagonjwa 17,Sonona wagonjwa 12 huku madawa ya kulevya wakiwa ni 15.
“Moja ya magonjwa yanayotokea kwa wingi ni ugonjwa wa kifafa na kimsingi zipo sababu nyingi linalochangia tatizo hili ikiwepo changamoto za kimazingira na wengine ni changamoto za kibailojia ambalo tatizo lipo kwenye familia zao”alisema Dkt,Stanley Mlay
Vile vile amesema sababu nyingine inayopelekea matatizo ya afya ya akili ni changamoto nyingi za kimaisha kwa wananchi wa wilaya hiyo.
“Utakuta mwingine ana migogoro ya kifamilia,wengine migogoro ya mahusiano na mwisho wa siku mtu anakosa furaha katika maisha yake kwa ujumla kichwa kinamuuma anashindwa kufanya kazi zake za kawaida hayo ni moja ya matatizo ambayo tunayo.lakini pia kuna wengine wapo kwenye matumizi mabaya ya vilevi bila kuzingatia taratibu za lishe”alisema Mlay
Aidha amesema halmashauri ya wilaya ya Ludewa imeendelea kujitahidi kutoa matibabu katika vituo vya afya vilivyopo katika maeneo mabali mbali kwasababu serikali ina wataalamu waliopewa mafunzo na kutoa huduma kwenye kliniki za afya ya akili na wagonjwa wengi wamekuwa wakipona na kuendelea na majukumu yao huku wachache wakipewa rufaa kwa ajili uchunguzi sehemu za ubongo.
Dkt,Mlaya ametoa rai kwa wananchi kuzingatia utaratibu mzuri wa maisha kwa kuepukana na migogoro,kutafuta tiba mapema lakini kwa watumiaji wa vilevi kupunguza ili kuepukana kabisa na matatizo ya afya ya akili.
Enosent Mtweve ni mwenyekiti wa kijiji cha Mdilidili kata ya Lugarawa amekiri uwepo wagonjwa wa afya ya akili katika wilaya hiyo huku katika kijiji chake wakibainika wagonjwa zaidi ya 5 walioendelea kupata matibabu mbali mbali huku mmoja akiwa na tatizo kubwa zaidi hali iliyopelekea kumsaidia matibabu kwa ukaribu zaidi.
“Mgonjwa mmoja anayeonekana ana matatizo zaidi tumemsaidia kwa kuwasiliana na viongozi wa serikali lakini tumemkatia bima ya afya ili asitibiwe kwa usumbufu na imebainika toka utoto wake alikuwa na kifafa na baadaye amekuwa na matatizo makubwa ya afya ya akili,nashauli wananchi wetu pale wanapoona tatizo wawahi kwenda vituo vya afya”alisema Enosent Mtweve
Devotha Haule ni mwalimu wa shule ya msingi Kimelembe na Thomas Kayombo ni mkazi wa Ludewa mjini,wamesema ipo haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuepukana na vyanzo vya matatizo ya afya ya akili kwa kuwa katika mazingira yao wananchi wamekuwa wakikumbwa na matatizo kwa ukosefu wa elimu.
“Naomba wazazi tuzingatia hata ule mlo kamili kwa watoto kwa kuzingatia virutubisho kamili,na pia tuendelea kutoa elimu kwa mfano pale Kimelembe kuna kijana alisoma mpaka sekondari vizuri lakini sahizi amechanganyikiwa utakuta amevaa soksi rangi tofauti kuja kuulizia wanasema ameathrika na madawa ya kulevya”alisema Devotha Haule.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Dkt,Stanley Mlay akieleza namna halmashauri yake inavyopambana kukabiliana na matatizo ya afya ya akili na kuwataka wakazi wa Ludewa kufuata taratibu za maishi ili kuepukana na matatizo hayo.
No comments: