KITUO CHA UTAMADUNI CHA UFARANSA JIJINI DAR WAANDAA MAONESHO KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WASANII mbalimbali nchini Desemba 10 mwaka huu katika Kituo cha Utamaduni Ufaransa jijini Dar es Salaam wanatarajia kuonesha sanaa zao mbalimbali ambazo zinazungumzia na kuelezea mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsi nchini.
Aidha viongozi mbalimbali wakiwemo mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiongozwa na mwenyeji wao Balozi wa Ufaransaa nchini Tanzania watahudhuria katika siku hiyo ya kupinga ukatili wa kijinsia ambapo mbali ya wasanii kutakuwa na maonesho ya wajasiriamali mbalimbali watakaonesha kazi zao.
Akizungumza leo Desemba 8,2020 akiwa katika Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa jijini Dar es Salaam,Msanii Carola Kinasha amesema katika kuelekea siku hiyo wameamua kukutana na waandishi wa habari kuzungumzia umuhimu wa siku hiyo na matarajo yao watu 500 watahudhuria kushuhudia matukio yaliyoandaliwa katika kupinga ukatili kijinsia.
"Kutakuwa na matukio mengi ambayo yatafanyika katika siku hiyo ya Desemba 10,2020, mbali ya wasanii kuonesha kazi zao za sanaa zinazozungumzia masuala ya ukatili wa kijinsia, pia kutakuwa na maonesho ya wajasiriamali.Aidha Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya watoa tohuba zao,"amesema.
Amefafanua kama inavyojulikana siku ya kupinga ukatili wa kijinsia ni siku ya kidunia, hivyo wataitumia katika kueleza mipango na mikakati katika kukomesha ukatili wa kijinsia huku akieleza wazi ili kushinda mapambano hayo ni jukumu la watu wote, hivyo ametoa rai kwa wanaume nao kushiriki siku hiyo kwa kufika katika kituo hicho cha utamaduni.
Aidha amesema kuwatakuwa na wanawake maalum wanne watakaopata fursa ya kuonesha kazi zao za sanaa (filamu fupi)pamoja na kupata fursa ya kuzungumza chochote kuhusu kile ambacho wanakifanya.
Amesema tukio hilo litaanza saa 12 jioni hadi saa sita usiku ambapo miongoni mwa wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu."Tunawaomba waandishi wa habari mliopo hapa mtusaidie kufikisha taarifa hizi, tunatarajia kuwa na watu wengi siku hiyo, ni siku muhimu kwetu sote, hivyo tunawakaribisha wote."
No comments: