TANCDA YASEMA KUNA MUINGILIANO MKUBWA WA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NA YA KUAMBUKIZA
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SHIRIKISHO la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza(TANCDA)umesema hivi sasa kuna muingiliano mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza na yale ya kuambukiza huku ikifafanua kasi ya magonjywa yasiyoambukiza imekuwa kubwa katika jamii kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya mtindo wa maisha.
Hayo yamesemwa leo Desemba 8,2020 jijini Dar es Salaam na Mratibu wa TANCDA Happy Nchimbi wakati akizungumza na Michuzi TV na Michuzi Blog baada ya kumalizika kwa semina iliyoandaliwa kwa waandishi wa habari nchini kwa lengo la kujengewa uwezo kuhusu kufahamu kwa kina magonjwa yasiyoambukiza na sababu za magonjwa hayo.Pia kujengewa uwezo wa kufahamu muingiliano uliopo kati ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya kuambukiza.
"Tumekutana hapa leo na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini kwa dhumuni la kuwajengea uwezo kuhusu kufahamu kwa kina magonjwa yasiyoambukiza.Pia kufahamu muingiliano kati ya magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyoakumbukiza kwasababu muingiliano upo na mkubwa.
"Na wagonjwa wenye wenye magonjwa yasiyoakuambukiza wengi wanapata changamoto ya magonjwa ya kuambukiza na mara nyingi inakuwa shida.Hivyo tumewaita hapa kuwaeleza kunamuingiliano wa magonjwa yasiyoambukiza na ya kuambukiza na jitihada kubwa ambazo zinafanywa na shirika hilo katika kuhakikisha kunakuwa na uelewa kuhusu magonjwa hayo,"amesema.
Aidha amesema kwa sasa Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kunakuwa na Kliniki maalumu kwa wagonjwa wote ambao wana magonjwa sugu, lengo ni kuhakikisha mtu anapokwenda katika kliniki hiyo anamalizana na magonjwa mengine yote anayosumbuana nayo akiwa eneo moja.
Alipoulizwa kasi ya magonjwa yasiyoambukiza ikoje kwa hivi sasa, amejibu hali ya magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa japokuwa hawajafanya tafiti hizi karibuni kuonesha lakini tafiti ndogondogo ambazo zinazifanywa na shirikisho hilo zinaonesha kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza hasa wagonjwa wa moyo na sukari.
"Lakini kwa kushirikiana na Serikali tunaandaa mpango ambao tutakuja kufanya tafiti kubwa ambayo itakuwa jumuishi na itawakilisha nchi kwa Tanzania nzima kujua kwa sasa hali ikoje, lakini tuna takwimu za mwaka 2012 ambazo zinaonesha wagonjwa kisukari.
"Takwimu hizo zinaonesha asilimia tisa ya watanzania wanasumbuliwa na ugonjwa sukari na asilimia 26 wanaishi na magonjwa ya shinikizo la juu la damu,"amesema.
Awali Muuguzi Mwandamizi Mshauri kutoka Chama cha Kisukari Tanzania Eliezabeth Lifofo amezungumzia ugonjwa kisukari ambapo amesema wameugawa katika makundi matatu,kundi la kwanza ni la watoto wenye umri kuanzia 0 hadi miaka 30.
"Hawa tunawaweka kwenye kundi la kwanza la watoto, hawa wamepata shida kwamba ngongosho lao halitengezi dawa ya Inswilini ambayo inagawa sukari mwilini na wanaishi kwa kuchoma sindano kila siku katika maisha yao yote.
"Kundi la pili ni watu wazima ambao wao wanaweza kumeza vidonge kwasababu ngongosho lao linatengenza Iswilini ya kugawa sukari mwilini, lakini kuna mawili aidha Iswilini haifanyi kazi vizuri au inafanya kazi kiasi.Ugonjwa wa sukari aina ya tatu ni ule ambao unaathiri akina mama wajawazito ambao umri wa kubeba mimba umeanzia miaka 24,"amesema.
Amefafanua kwenye suala la kisukari kwa watoto ni changamoto kubwa kutokana na familia nyingi kuwatenga watoto wadogo kwani familia nyingi wazazi hufarakana kutokana na kina baba wengi kudai watoto walizaliwa na sukari sio wa kwao kwasababu tu mtoto amezaliwa na kisukari.
"Wakati hili ni tatizo la jamii na inapaswa kufahamu mtoto amepata ugonjwa wa sukari ni kutokana na ngongosho lake halitengenezi dawa ya Inswilini na Inswilini kazi yake ni kugawa sukari mwilini na si kwamba huyu mama ameenda sehemu nyingine amepata ujauzito huo,
Aidha amezungumzia ulaji mwingi wa mafuta ambavyo nao umekuwa ukichagia kusababisha magonjwa yasiyoambukiza katika mwili wa binadamu, hivyo ametoa rai kwa jamii kupunguza ulaji mwingi wa mafuta kwani una madhara makubwa.
"Mafuta ni mojawapo ya visababishi vya kupata magonjwa yasiyoambukiza, mafuta mengi mwilini husababisha shinikizo la damu, hivyo jamii inatakiwa kutumia mafuta kidogo sana.Umuhimu wa mafuta upo kwasababu ila yawe kiasi.
"Bila mafuta chakula unakuta vitamini za aina nne haziingii mwilini, vitamini A, vitamini B, vitamini K na vitamini E, hizo vitamini zinaingia mwilini endapo chakula kinamfuta lakini yawe kidogo yasiwe mengi,"amesema Lifofo.
Hivyo amependekeza katika familia ya watu wa nne ni vema mafuta ambayo yatatumika kwa mwezi yasiwe zaidi ya chupa ndogo ya maji ya kubwa yenye ujazo wa Mil 600.
Aidha ameshauri jamii kuachana na tabia ya kutumia zaidi ya mara moja mafuta ambayo yametumika kwani madhara yake ni makubwa yakiwemo ya kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama kansa ya utumbo.
Muuguzi Mwandamizi Mshauri kutoka Chama cha Kisukari Tanzania Eliezabeth Lifofo akielezea sababu mbalimbali zinazosababisha magonjwa yasiyoambukiza katika mwili wa binadamu ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa jamii kujiepusha na matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula.
Mwenyekiti wa Chama Waandishi wa Habari wa Magonjwa Yasiyoambukiza (TOANCD) Leon Bahati akifafanua jambo.
Mwandishi Herrieth Makweta akizungumza jambo wakati wa semina hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Magonywa ya Moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete (JKCI) Dk.Tatizo Wanne akizungumza wakati wa semina hiyo iliyoandaliwa kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kwenye semina ya kujengewa uelewa wa magonjwa yasiambukiza iliyoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania(TANCDA).Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI).
Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania(TANCDA)Happy Nchimbi akizungumza jambo wakati wa semina iliyoandaliwa na shirikisho hilo kwa waandishi wa habari nchini ikiwa ni mkakati wa kuendelea kujengeana uwezo kufahamu kuhusu magonjwa yasiambukiza na sabababu zake.
No comments: