KISARAWE WAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU UJENZI WA MADARASA,DC JOKATE ATOA NENO



Na Said Mwishehe,Michuzi Blog

WAKATI Watanzania wakisherehekea Siku ya Uhuru wa Tanganyika ambayo hufanyika kila ifikapo Desemba 9, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo ameitumia siku hiyo kushiriki kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Janguo,Mloganzila na ujenzi wa mradi mkubwa wa Shule ya Sekondari ya Wilaya ya Kisarawe ambao utagharimu Sh.milioni 700.

Katika kukagua na kushiriki ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo Jokate aliambatana na viongozi wengine wa halmashauri hiyo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Mussa Gama ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Serikali kupitia maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

 Ambapo imeagiza viongozi wote wa halmashauri hakuna kwenda likizo na badala yake wahakikishe wanatumia kipindi hiki kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba 2020  wajiunge na kidato cha kwanza ifikapo Januari mwaka 2021.

Akizungumza leo Desemba 9,2020 Jocate amesema wameamua kuitumia siku hiyo ambayo Watanzania tunaadhimisha miaka 59 ya nchi yetu kupata Uhuru wake kwa kuangalia eneo la sekta ya elimu na hasa katika kutatua changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza, na kwamba mwaka huu Kisawe waliofauli ni wanafunzi 2488.

Hivyo katika kutekeleza agizo hilo, Kisarawe tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wote waliofauli katika Wilaya ya Kisarawe ifikapo Januari mwakani shule zinapofunguliwa wakute vyumba vya madarasa vipo.

Akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa Sekondari ya Wilaya ya Kisarawe ambayo itagharimu kiasi cha Sh.milioni 700, Jokate amesema kimsingi ujenzi wa sekondari hiyo unakwenda kuondoa changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu wa kwenda na kurudi shuleni.

 "Kata hii ya Kazimzumbwi ilikuwa na chagamoto ya kukosa shule ya Sekondari,  ukipita barabarani unakutana na wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.Umbali huo umesababisha wawe wanaingia darasani saa tatu asubuhi na huwezi kuwahukumu kutokana na hali halisi ya umbali uliyopo wa kufika shule.

"Hivyo niseme kwa wana Kazimzumbwi ninafuraha nyingi sana kupata mradi huu wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ambao utagharimu Sh.milioni 700 na shule hii ndio inabeba jina la Wilaya ya Kisarawe, shule hii itakuwa na madarasa nane, matundu ya vyoo, maabara,bwalo,nyumba za walimu na ofisi.

"Kwa kweli tunakwenda kujenga shule ambayo itatoa taaswira mpya ya mji wa Kisarawe na hii inatokana na juhudi za Mheshimiwa Bunge wetu ambaye ameepishwa tena Selemani Jafo aliyesema anakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya kuelekeza katika shule hiyo itakayokuwa ya mfano katika wilaya ya kisarawe. Na kwasababu itakuwa mfano na kubeba taaswira ya wilaya yetu ndio maana itabeba jina la Kisarawe,"amesema.

 Ameongeza mafanikio ya mradi huo yapo kwenye mikono ya wananchi na iwapo mradi utakwama nao utakuwa umekwamishwa na wananchi."Kwasababu tumeanza vizuri na Mkurugenzi ametoa taarifa alifika hapa ,wakakaa na wananchi na viongozi wa Chama na Serikali na kwa pamoja wakatafuta eneo ambalo shule itajengwa, kwa hiyo jambo hili limekuwa shirikishi, hivyo ni vema tukaanza pamoja na kumaliza pamoja.

"Ni imani yangu na kutokana na umuhimu huu tumeamua kutafuta kikosi kazi kutoka Jeshi la Polisi ambacho kitapiga kambi kujenga sekondari yetu hii na itakapofika Januari mwakani madarasa yaanze kutumika kwa kupokea wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza.Wilaya ya Kisarawe jumla ya wanafunzi 2,488 wamefaulu kuingia kidato cha kwanza na wote lazima waende shule".

Aidha amewaomba wananchi kuwa walinzi kwa kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinakuwa salama na hakuna sababu ya wananchi kuutia dosari mradi huo wa ujenzi wa sekondari ya Kisarawe na kwamba ujenzi wa sekondari hiyo ni muhimu na itakuwa na jengo la ghorofa ,

 "Wananchi wana kila sababu ya kuubeba mradi huu na washirikiane na waliopewa jukumu la kuujenga.Mafanikio ya mradi yabebe jasho na damu ya kila mmoja wetu.Lakini nitoe rai tukapoanza kupokea wanafunzi tuhakikishe kunakuwa na nidhamu kuanzia wanafunzi pamoja na walimu wote."

 Kwa upande wake Msimamizi wa ujenzi wa Sekondari hiyo itakayopewa jina la Sekondari ya Kisarawe kutoka Jeshi la Polisi Sajenti Herman Mayala amemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwamba ujenzi wa sekondari  hiyo utakamilika kwa wakati na wanafunzi wataingia shuleni kama ratiba ya kufungua shule inavyooleza.

 "Na ndio maana tumepiga kambi hapa kuhakikisha tunajenga usiku na mchana , hatulala ,tutafanya ujenzi wakati wote.Nakuhakikishia Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ,ujenzi wa shule utakamilika kwa wakati na wanafunzi wataanza masomo yao kama kawaida Tumejipanga na tuko tayari kuifanya kazi hii kwa ubora mkubwa,"amesema Mayala.

 Awali Mkuu wa Wilaya ya kisarawe ameshiriki kwa hatua ya awali ya ujenzi wa madarasa mawili katika Sekondari ya Jenguo iliyopo Kata ya Msanga ikiwa ni kuanza kutekeleza kwa kauli ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ya kutaka halmashauri nchi kujenga vyumba vya madarasa ili watoto wote waliofaulu waweze kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari 2021.

 Amesema katika halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kuna upungufu wa madarasa saba na kati ya hayo madarasa mawili ni kutoka Shule ya Sekondari Jenguo,hivyo amewapongeza wananchi na Mwalimu Mkuu kwa uamuzi wao wa kuanzisha ujenzi wa vyumba hivyo.

 "Nimefurahishwa na wananchi kwa jinsi mabavyo wameona umuhimu wa elimu kwa kuhakikisha wanatoa fedha Sh.milioni tano wa ajili ya kuanza ujenzi, nami kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya nitachangia Sh.milioni 15.Nataka madarasa haya hadi inapofikia Desemba 30 mwaka huu yawe yamekamilika na ifikapo Januari 2021 watoto waingie darasani kusoma.Shule zitafunguliwa Januari 11, mwaka 2021,"amesema.

 Ameongeza kwamba kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali kupitia Waziri Mkuu , hakuna likizo,hivyo wao Kisarawe wameona watumie siku hii ya 9 Desemba kushiriki katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kutoa fursa kwa watoto kupata nafasi ya kujiunga na msomo katika muhula mpya wa masomo.

 Aidha amepongeza juhudi za wananchi wa Kata ya Msanga kwa kuona umuhimu wa madarasa kwani kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe Mussa Gama, kuanzia mwaka wa masomo 2018 kulikuwa na ongezeko la wanafunzi 145, mwaka 2019 wanafunzi 150 na mwaka 2020 lilikuwa 219 na mwaka huu kuelekea 2021 ongezeko ni wanafunzi 190, hivyo nawapongeza wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.

 Wakati huo huo akiwa katika sekondari ya Janguo kwa kufanikisha upatikanaji wa madawati 87 na hiyo ni kutokana na makubaliano ya wazazi ambao kwa hiyaro yao waliamua kuchangia Sh 5,000.

Jokate pia ametembelea Shule ya Sekondari Mlonganzila ambako nako kuna ujenzi wa madarasa manne unaendelea kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu  wanakwenda shuleni ifikapo Januari.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo akizungumza na wananchi baada kwenda kushiriki kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Janguo ambapo amewahakikishia wananchi kuwa wanafunzi wote ambao wanatarajia kuanza kidato cha kwanza mwakani wote wanakwenda shule.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo akikata mzizi wakati akishiriki kuchimba msingi katika ujenzi wa chumba cha dasarasa katika Sekondari ya Jenguo.Aliyejifunga kitambaa kichwani ni Katibu Tawala Wilaya ya Kisarawe Mwanana Msumi aliyekuwa akichota mchanga.

Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe akiendelea na kazi ya kuchimba udongo ili kuashiria kuanza kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Sekondari ya Jenguo ikiwa ni mkakati wa kuanza kutekeleza agizo la Serikali la kujengwa vyumba vya madarasa.

Baadhi ya wananchi waliokuwa wakishiriki kwenye kuchimba msingi ili kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Jenguo wakimpiga makofi Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo baada ya kufika shuleni hapo kushuhudia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo(kulia) akipiga makofi baada ya kufurahishwa na maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Jenguo(hayuko pichani).Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mwanana Msumi akiwa makini kufuatilia maelezo hayo.

Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Jenguo baada ya kumaliza kuchimba msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jenguo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo na Mkurugenzi wa Wilaya hiyo kufika shuleni hapo kushiriki ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa


Sehemu ya mafundi waliokuwa kwenye ujenzi wa Shule ya Sekondari Kisarawe wakiendelea na majukumu ya ujenzi huo ambao umeanza leo ambapo jumla ya Sh.milioni 700 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo.

 

Msimamizi wa ujenzi wa sekondari ya Kisarawe  Herman Mayala kutoka Jeshi la Polisi akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo baada ya kufika katika eneo hilo la mradi wa ujenzi wa shule hiyo.Mayala amemhakikishia Jokate kwamba ujenzi utakamilika haraka na wanafunzi wataingia darasani ifikapo Januari mwakani.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kazimzumbwi wilayani Kisarawe wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo baada ya kutembelea katika eneo hilo kuangalia shughuli za ujenzi wa sekondari ya Kisarawe.

 

No comments: