Ukata wadaiwa kusabaisha madereva utalii kutelekeza familia

Na Seif Mangwangi, Arusha 

UKOSEFU wa ajira katika sekta ya utalii nchini kumeelezwa kusababisha baadhi ya wafanyakazi waliokuwa wakifanyakazi katika kampuni za utalii pamoja na kuhudumu kwenye hoteli mbalimbali za kitalii Jijini Arusha kutelekeza familia.

Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake, mmoja wa madereva wa utalii jijini Arusha amesema kuwa tangu kulipolipuka kwa ugonjwa wa Corona nchini, wafanyakazi katika kampuni za utalii walipunguzwa na zingine zilifunga.

Alisema kutokana na ukata uliowakumba kwa zaidi ya miezi kumi sasa, amelazimika kumrudisha mke kwa wazazi wake huku watoto akiwapeleka kijijini kwa wazazi wake baada ya kukosa fedha za kujikimu na kuhudumia familia.

Kutokana na ukata huo, anasema amelazimika kufanya kazi za kusaidia fundi kwenye sekta ya ujenzi wa nyumba na kupata fedha kidogo ambayo imekuwa ikimsaidia kupata mlo lakini pia kulipia kodi ya pango la nyumba katika chumba kimoja alichokipanga maeneo ya Kwa mromboo nje kidogo ya jiji la Arusha.

“Ndugu yangu madhara ya Corona ni makubwa sana, sisi watu wa utalii tulifikiri ni masihara lakini ukweli hali ni mbaya sana, nimelazimika kumrudisha mke wangu kwao kwa sababu kwa kweli sina kipato cha kuendelea kumtunza kwa sasa na watoto nimewapeleka kijijini kwa wazazi wangu,”anasema.

Kwa upande wake Edward Selasini, mkazi wa Arusha ambaye amekuwa akijishughulisha na shughuli za utalii anasema kuwa sekta ya utalii imepata pigo kubwa sana baada ya wengi wa wafanyakazi waliokuwa wameajiriwa kujikuta wakilazimika kufanyakazi ambazo hawajawahi kuzifanya hapo mwazo ili kujikimu kimaisha.

“Baada ya utalii kuanguka ninao rafiki zangu wengi sana wamejikuta wakianza kutafuta kazi pasipokufanikiwa na wengine wamejiingiza kwenye kilimo na wengine wameanza kufuga mifugo midogo midogo kama kuku na kuuza,”anasema.

Anasema kutokana na hali ya maisha kuwa mbaya kwa wafanyakazi walikuwa katika sekta ya utalii, anaiomba Serikali kuangalia namna ya kuweza kusaidia sekta hiyo ikiwemo kutoa mikopo itakayowawezesha kufanya biashara na kupata kipato cha kujikimu.


 

No comments: