SIMBA SC YAISHANGAZA PLATEAU CAF CL, LICHA YA MECHI KUZUIWA ‘LIVE’


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

LICHA ya kuwekewa vikwazo kwa mtanange wao kurushwa Mubashara (Live), Klabu ya Soka ya Simba imetanguliza mguu mmoja kusonga mbele katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyewe wao Plateau United ya Nigeria katika mchezo uliopigwa katika dimba la New Jos nchini humo.

Katika mchezo huo Tripple C, Clautos Chota Chama, Mwamba wa Lusaka Nyota wa Simba SC alipeleka simanzi, majonzi kwa Wanigeria, Plateau United katika dakika ya 54 baada ya kupokea pasi safi (Assist) ya Mshambuliaji, Lous Jose Miquissone. 

Mchezo huo uliokuwa wa kasi dakika zote 90, Simba SC walionekana kucheza kwa tahadhari kubwa na kuheshimu wapinzani wao waliokuwa katika dimba la nyumbani sambamba na kuwashambulia kwa mtindo wa Mashambulizi ya Kushtukiza (Counter Attack).

Hata hivyo, Simba SC walifanya mabadiliko kwa kumtoa Beki Joash Onyango (Aliyeumia) na nafasi yake kuchukuliwa na Kiungo, Mzamiru Yassin na kutolewa Hassan Dilunga nafasi yake kuchukuliwa na Bernard Morrison aliyeingia Kipindi cha Pili na Ibrahim Ame aliyeingia kuchukua nafasi ya Clatous Chama.

Simba SC ili kusonga mbele Raundi ya Pili katika Michuano hiyo wanasubiri mchezo wa marudiano utakaopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa, Desemba 5 mwaka huu.

No comments: