RITA YAKUTANA NA WADAU KUPANGA MIKAKATI YA KUSAJILI WATOTO MIKOA YA MIPAKANI

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umekutana na wadau wa  Usajili wa Matukio muhimu ya Binadamu na Takwimu na masuala ya utambuzi na kukubaliana kufanya kazi kwa pamoja na kuweka mikakati madhubuti itakayowezesha kusajili vizazi katika maeneo ya Mikoa inayopakana na nchi jirani bila ya kuathiri sheria na usalama wa nchi.

 Taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Ofisi ya Raisi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Tifa (NIDA) pamoja na wawakilishi kutoka baadhi ya mikoa inatotekeleza Mpango wa Usajili wa Watoto.

Akifungua Mkutano huo wa siku mbili hii leo Jijini Arusha, Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bi Emmy Hudson amesema RITA inaendelea kutekeleza Mpango wa Usajili wa Watoto walio na Umri Chini ya miaka mitano na mikoa iliyosalia katika utekelezaji wa mpango huu ina muingiliano mkubwa na wananchi kutoka nchi jirani hivyo Wakala umeona ni vyema kukutana na wadau wote ili kufanya tathmini ya kina ya tulikotoka na kuweka mikakati ya mikoa saba iliyobakia kuanza utekelezaji wa Mkakati huu ambayo ni Arusha, Manyara, Kigoma, Kagera, Katavi, Rukwa na Tabora. 

Taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Ofisi ya Raisi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) pamoja na wawakilishi kutoka baadhi ya mikoa inatotekeleza Mpango wa Usajili wa Watoto.

 Katika maelezo yake ya awali Bi Hudson amesema Serikali imefanya maboresho makubwa katika mfumo wa Usajili kwa kubuni Mkakati wa Usajili wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu ambao umeanza kutekelezwa kupitia Mpango wa usajili wa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ambao mpaka sasa umeshaanza kutekelezwa katika mikoa 18 na kuonusha mafanikio makubwa kwa kuweza kuwasajili watoto zaidi ya  Milioni 5 na kuongeza idadi ya watoto waliosajiliwa nchini kutoka asilimia 13 mpaka kufikia asilimia 49.  

Bi Hudson ameongeza kuwa kutokana na maboresho mbalimbali yanayofanyika yameiwezesha wakala kuweza kupata takwimu kwa wakati kupitia mifumo ya kiteknolojia na kwa sasa tunajivunia kwamba tumeanza kuunganishwa mifumo ya Taasisi nyingine za usajili na utambuzi wa wananchi hivyo kuwezesha kubadilishana taarifa. 

Mkurugenzi Msaidizi – Ustawi wa Jamii kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI Bw Rashid Maftah ameipongeza RITA kwa kuamua kugatua majukumu ya usajili kwenda Serikali za Mitaa kwani imewezesha wananchi kupatiwa huduma hiyo jirani na maeneo wanayoishi hivyo kuwezesha kupatikana kwa takwimu sahihi na kwa wakati ambazo ni muhimu katika kupanga mipango ya maendeleo.

 Ameongeza kwamba kwa sasa Ofisi yake inashirikiana kwa karibu na RITA katika utekelezaji wa Mpango wa Usajili wa Watoto hivyo kuwezesha kuongeza kiwango cha usajili. Kwa upande wa Usajili maeneo ya mipakani ameshauri kushirikisha kamati za ulinzi na usalama ambazo zipo mpaka ngazi za mitaa na vijiji. Pia alishauri kutumia Daftari la Wakazi wa Kijiji kwa ajili ya kufanya uhakiki.

Naye Meneja Utambuzi na Usajili Kutoka NIDA Bi Julien Mafuru alieleza mikakati iliyotumiwa na taasisi yake katika maeneo ya mipakani na kuongeza kwamba maeneo mengi wananchi wameshaajiliwa hivyo RITA na taasisi nyingine wanaweza kutumia taarifa zilizopo kuwatambua wazazi wa watoto watakaosajiliwa.

RITA inatekeleza Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano kwa kushirikiana na Wadau ambao ni  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Serikali ya Canada na Kampuni ya Simu za Mkononi ya TIGO.Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu Bi Emmy Hudson akiwasilisha hutuba ya ufunguzi wa Kikao cha wadau wa masuala ya utambuzi wa watu na usajili wa matukio muhimu ya Binadamu na Takwimu hii leo Jijini Arusha.Mchumi Mwandamizi, Bi Happyness Mugyabuso kutoa ofisi ya Waziri Mkuu akifafanua umuhimu wa kusajili matukio ya vizazi na vifo ndoa na talaka katika upangaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

Wajumbe wa mkutano wakifuatilia majadiliano.

No comments: