Mkoa wa Ruvuma una mbolea ya kutosha msimu mzima

Mbolea iliyohifadhiwa katika ghala la SONAMCU mjini Songea.
Mbolea iliyoifadhiwa katika ghala ya kuhifadhia mbolea la SONAMCU mjini Songea.
Mbolea ya SA iliyohifadhiwa katika ghala la SONAMCU mjini Songea.
Mkurugenzi Mtendaji wa NFRA Dkt.Stephan Ngailo akizungumza baada ya kukagua ghala la kuhifadhia mbolea la SONAMCU mjini Songea.

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (NFRA) Dkt.Stephan Ngailo amesema Mkoa wa Ruvuma una mbolea ya kutosha ya aina zote itakayokidhi mahitaji ya wakulima katika msimu mzima.

Akizungumza wakati anakagua ghala la mbolea la SONAMCU mjini Songea,Dkt.Ngailo amesema amekagua maghala ya mbolea katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma na ameridhika kuwa mbolea ipo ya kutosha.

Ametoa rai kwa wakulima kuendelea kujiandaa kununua mbegu na kulima mashamba yao ambapo amesema mbolea zote zipo za kutosha ikiwemo urea,DP,SA na NPK.

Amesema serikali imekusudia kuhakikisha kuwa mbolea za aina zote zinapatikana katika mikoa inayolima mazao ya chakula ukiwemo Mkoa wa Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Rukwa, Katavi,Kigoma na Tabora na kwamba serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa maeneo hayo yote yanapata mbolea ya kutosha.

“Katika nchi nzima tuna zaidi ya asilimia 60 ya mahitaji yote ya mbolea,tunatarajia kufikia kati ya mwezi Februari hadi Machi tutakuwa na asilimia 75 hadi 80 ya mahitaji yote ya mbolea nchini’’,amesisitiza Dkt.Ngailo.

Dkt.Ngailo amesema katika msimu huu,serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli imejipanga vizuri kuhakikisha wakulima wanapata mbolea za aina zote kwa wakati.

Hata hivyo amesema katika tathmini iliyofanyika Oktoba mwaka huu,Tanzania ilikuwa na tani zaidi ya 65,000 za mbolea ya urea na kwa mbolea nyingine zote zilifikia tani 252,000 ambapo kiasi hicho cha mbolea kinaweza kufika hadi mwezi Februri 2021.

Ameongeza kuwa hivi sasa katika bandari ya Dar es salaam kuna meli imetia nanga inaendelea kupakua mbolea aina ya urea tani 18,000 na kuna tani nyingine za mbolea zinatarajiwa kuingizwa nchini wakati wowote.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Paulo Msemwa amesema mahitaji ya mbolea katika Mkoa ni tani zaidi ya 50,000 ambapo hadi sasa zimeingia tani zaidi ya 13,000 .

Amesema mbolea imesambazwa katika maeneo yote ya Mkoa hivyo ametoa rai kwa wakulima kuandaa mapema pembejeo zote za kilimo ili kuongeza uzalishaji. 

Mkoa wa Ruvuma katika misimu miwili mfululizo ya 2018/2019 na 2019/2020 umeongoza na kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula,huku sababu kubwa ya kuongeza uzalishaji ni upatikanaji wa mbolea ya kutosha.

Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Novemba 13,2020

No comments: