Pori la Akiba Liparamba limesheni vivutio vya utalii vya kila aina
Pori la wanyamapori Liparamba lililopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ni miongoni mwa mapori yaliyopitiwa na ushoroba wa wanyama.
Afisa Utalii wa Pori hilo Maajabu Mbogo amesema pori hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2000,limebahatika kuwa na wanyamapori wakubwa na wadogo wakiwemo tembo,simba, chuo,viboko,mamba,tandala,pofu,palahala,kuro,nyati, pundamilia,fisi,chui na mbweha na ndege kama vile kanga, koribustard(Mbawala) na fundichuma.
“Neno liparamba ni la kabila la kimatengo ambao ni wenyeji wanaoishi wilaya ya Mbinga,maana liparamba ni mbuzimawe,pori hili lina makundi makubwa ya tembo,ambao ni wakimbizi kwa sababu huwa wanatoka Msumbiji na kuhamia Liparamba’’,alisema Mbogo.
Amesema makundi makubwa ya tembo kutoka Msumbiji wanaanza kuingia kwa wingi katika pori la Liparamba kuanzia mwezi Machi kila mwaka na kufikia mwezi Julai,tembo wanaanza kurudi nchini Msumbiji na kwamba inapofika kati ya Septemba na Oktoba wanabaki tembo wachache sana ndani ya hifadhi hiyo.
“Inapotokea kule nchini Msumbiji majangili yamewashambulia tembo au kuwasumbua,tembo hao wanapoingia katika hifadhi ya Liparamba hawatoki,wanaweza ndani ya pori la Liparamba kati ya miaka miwili hadi mitatu bila kutoka na kurudi Msumbiji kwa sababu Liparamba ni sehemu salama ya kuishi tembo.’’alisisitiza.
Amesema katika pori la Liparamba pia amewahi kuonekana simba mweupe na kwamba jambo hilo sio kitu cha ajabu sana kwa kuwa viumbe hai wakiwemo wanyama na mimea ikipata kasoro kwenye ngozi au majani inaweza kuwa na rangi nyeupe.
Anavitaja vivutio vingine vilivyopo katika pori hilo ni uwepo wa aina mbalimbali za nyoka kama vile jamii ya mamba na kobra na kwamba pori hilo lina maporomoko ya maji ya Nakatuta katika Mto Ruvuma ambayo ni kivutio cha asili cha utalii.
Kwa mujibu wa Afisa Utalii huyo,pori hilo lina vivutio vinavyofaa kufanya utalii wa kupanda kwenye mawe kwa sababu ndani ya hifadhi hiyo,kuna mawe makubwa yanayofaa kwa utalii wa aina hiyo.
Amesema ndani ya pori hilo kuna miti ya ajabu ukiwemo mti wa mtetereka ambao ukikauka unabadilika na kuwa jiwe na kwamba miti ya aina hiyo ipo kwa wingi katika eneo la Nakatuta kandokando mwa Mto Ruvuma hivyo kuvutia watalii wengi wanaopenda kufanya utafiti wa miti na mimea.
Katika eneo la Mkuyu ndani ya pori la Liparamba pia kuna kivutio kinachowashangaza wengi ambacho,maji yanayotiririka kwenye mto Mkuyu yametengeneza mfano wa ramani ya Afrika juu ya mwamba.
“Maji yameweza kutengeneza mfano wa ramani ya Afrika juu ya mwamba,ukichukua ramani ya Afrika na kuangalia ramani iliyotengezwa na maji hakuna tofauti ni ramani kabisa ya Afrika,haya ni moja ya maajabu katika pori la Liparamba’’,alisema Mbogo.
Kwa upande wake Mhifadhi Msaidizi wa pori hilo Paul Protas anakitaja kivutio kingine kilichopo katika pori hilo ni uwepo wa ndege aina ya koribustard(Mbawala) ambaye hapa nchini anatumika kama alama ya Taifa kama ilivyo kwa mnayama twiga.
“Huyu ni ndege mkubwa ana uwezo wa kufikisha uzito KG 16,ana urefu wa SM 1330,huyu ni ndege wa kitaifa,anachinjwa kwa kibali kinachoombwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’,anasisitiza.
Kwa upande wake Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema pori hilo lina kiwango cha juu cha hifadhi ambacho kinatiliwa mkazo kisheria katika ulinzi,usimamizi, uendelezaji na matumizi ya busara ya mali hai ikiwemo misitu,samaki na wanyamapori.
Utafiti umebaini kuwa Liparamba ni eneo kipekee katika ukanda wa juu wa misitu ya miombo lenye msitu mnene wa asili na wenye mandhari ya kuvutia.
No comments: