DK MAGUFULI: TUTANUNUA NDEGE MPYA YA MIZIGO NA MELI NANE ZA UVUVI
Charles James, Michuzi TV
RAIS Dkt. John Magufuli amesema ndani ya miaka mitano inayokuja serikali yake imejipanga kununua ndege moja ya mizigo ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya bustani, minofu ya samaki na nyama lengo ni kuwafanya wakulima watajirike kutokana na kazi wanayofanya.
Dkt.Magufuli ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma ambapo anazindua rasmi Bunge la 12 sambamba na kulihutubia bunge hilo na Taifa kwa ujumla na kusisitiza kuwa lengo lake ni kuona kila mtanzania ananufaika na maendeleo ya ukuaji uchumi.
Amesema serikali yake imepanga kuongeza tija kwenye kilimo kwa kukifanya kuwa cha kibiashara lengo likiwa kuwa na hifadhi kubwa ya chakula, malighafi za viwandani na kuuza pia nje ya nchi hivyo upatikanaji wa mbegu na zana za kilimo zitaboreshwa.
Kwa upande wa uvuvi amesema licha ya kutoa mikopo ya uvuvi, kupitia upya tozo za uvivu sambamba na kuboresha zana za uvivu, serikali pia imepanga kununua meli kubwa nane za uvivu ili kusaidia uvuvi kwenye bahari kuu kwa upande wa Tanzania bara na visiwani Zanzibar.
" Kwenye miaka mitano hii Mawaziri wa Kilimo, Biashara, Uvuvi na Mambo ya Nje wanapaswa kuendelea kufanya kazi ya kuzihudumia sekta hizo ili zitoe unafuu wa maisha kwa watanzania waliojiajiri huko sambamba na kukuza pato la Taifa." Amesema Magufuli.
No comments: