NDUGAI AWATAKA WAHITIMU ELIMU YA JUU KUTUMIA VYEMA MAARIFA WALIYOYAPATA VYUONI


Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai (kushoto) akiwa ameambatana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Prof. Tadeo Satta wakiwasili katika Mahafali ya 46 chuo hicho yaliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai  akizungumza na Wahitimu wa Chuo cha  Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wakati wa  Mahafali ya 46 chuo hicho yaliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai  (wa pili kushoto) akimpatia zawadi Mwanafunzi Bora kwa Wahitimu wa kozi zote za Shahada wa  Chuo cha Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Bw. Robin Micky Goliama wakati wa  Mahafali ya 46 chuo hicho yaliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka  kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Tadeo Satta, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Prof. Emmanuel Mjema na Mwakilishi wa Waziri wa Fedha ambaye pia Naibu Mkurugenzi wa Mipango katika Wizara ya Fedha, Bw. David Mwankenja.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai (katikati) akizungumza na  Mkuu wa Chuo cha  Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta (kulia) na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Prof. Emmanuel Mjema (kushoto) wakati wa  Mahafali ya 46 chuo hicho yaliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai  (katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na Menejimenti  na Wanafunzi Bora katika kozi mbalimbali wa   Chuo cha Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wakati wa  Mahafali ya 46 chuo hicho yaliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amewataka wahitimu wa elimu ya juu kuwa wabunifu na kutumia maarifa waliyoyapata kujitengenezea fursa za kiuchumi kwa kujiajiri na kuajiri wengine.

Akizungumza katika mahafali ya 46 ya Chuo Cha usimamizi wa Fedha (IFM,) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam,  Ndugai amesema kuwa, uwekezaji wa wazazi kwa vijana katika sekta ya elimu ni mkubwa sana, hivyo ni vyema wakatumia maarifa katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

"Baadhi yenu mmepata ufadhili kutoka bodi ya mkopo na wengine mkawezeshwa na wazazi hadi mmefika hapa... wanasema ukibebwa bebeka  mkawe chachu ya maendeleo na wazalendo kwa Taifa." Amesema.

Aidha amesema, kumekuwa na mjadala wa muda mrefu wa kielimu bungeni na hata Rais mstaafu wa awamu ya tatu Hayati. Benjamin William Mkapa alipendekeza kuwepo kwa mjadala mkubwa wa elimu ya kujua ni nini kitapatikana kutoka kwa wahitimu.

" Ninawatakia heri katika maisha mnayoenda kuyaanza....mkawe bora katika jamii na taifa kwa ujumla." Ameeleza.

Vilevile Spika Ndugai amekipongeza Chuo Cha usimamizi wa Fedha (IFM) chini ya uongozi wa Prof. Tadeo Satta kwa kuendelea kutoa elimu bora katika Mikoa mbalimbali nchini na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha gurudumu la elimu linasonga mbele zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Tadeo Satta amesema, Chuo hicho kinaendeleza azma yake ya ujenzi wa taifa kwa kuhakikisha wanakomboa vijana wengi kupitia elimu.

Amesema, wataendelea kuwafikia wananchi kwa kuendelea kujenga matawi katika Mikoa mbalimbali ili vijana wapate maarifa yatakayowasaidia katika kujikomboa kiuchumi na ujenzi wa Taifa kwa ujumla.

No comments: