KIBOKO NA MKEWE WAKUTWA NA KESI YA KUJIBU
Uamuzi huo umetolewa leo Novemba 27, 2020 na mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi, jijini Dar es Salaam, baada ya upande wa mashtaka kufunga kesi yao kwa kuwaita mashahidi sita na vielelezo 16 yakiwemo magari matatu Toyota Prado, Toyota Hilux na Toyota Land Cruiser.
Akisoma uamuzi huo Jaji Lilian Mashaka aliyekuwa akimsikiliza kesi hiyo amesema, upande wa mashtaka umefunga kesi yao na Mahakama imefunga kwa upande wa mashtaka.
"Upande wa mashtaka kupitia mashahidi wao sita na vielelezo hivyo, wamaweza kuthibitisha kuwa kuna kosa washtakiwa mmetenda, hivyo mahakama imeona mnayo kesi ya kujibu lakini mna haki ya kutoa utetezi wenu chini ya kiapo na pia mnahaki ya kuleta mashahidi wenu, amesema Jaji Mashaka
Hata hivyo washtakiwa walipoulizwa watajitetetea kwa njia gani, mshtakiwa wa pili (Pilly) akaanza kuangua kilio lakini jaji alimtaka asilie bali ajipange kuja kutoa utetezi wake.
" Nakuomba usilie, hapa mmekuja kutafuta haki, unatakiwa ujipange uje ujitetee, ukilia sasa hivi haitasaidia, jipange utoe utetezi wako,"akasema Jaji Mashaka
Washtakiwa wamedai kuwa watajitetea kwa kiapo, ambapo Wakili wao, Majura Magafu amedai kuwa hawana cha kuongeza, lakini siku ya utetezi wao wataleta kadi za magari halisi.
Aidha, Wakili wa Serikali, Salim Msemo aliiomba Mahakama hiyo kama itaridhia gari hizo ziwe chini ya Mamlaka ya Kuzuia Dawa za Kulevya (DCEA) kutokana na hali ya magari hayo, ambapo Jaji alitaka jina la mtu ambae atayahifadhi hayo magari na sio ofisi.
"Nina mkabidhi Inspekta Hassan Msangi kielelezo P13, P14 na P15 kwa ajili ya kuhifadhi na anapaswa kuyaleta jumatatu, Novemba 3, Washtakiwa mtaendelea kuwa nchini ya uangalizi, mjiandae mje kutoa utetezi wenu," amesema
Shahidi wa mwisho kwa upande wa mashtaka katika kesi hiyo Raymond Kimambo ambaye ni jirani yake Kiboko, aliieleza Mahakama jinsi alivyoshuhudia upekuzi nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.
Mbali na wakili Msemo, mawakili wengine wa Serikali wanaoendesha kesi hiyo, Costantine Kakula na Candid Nasua.
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 29/2018, Kiboko na mkewe wanadaiwa, Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kuÄşevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu251.25.
No comments: