ASKOFU GWAJIMA AANZA KAZI KWA KISHINDO, KUTATUA JANGA LA VOLKANO KUNDUCHI
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MBUNGE wa Jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima ameanza rasmi kazi ya kuwatumikia Wananchi wa Jimbo hilo kwa kutembelea eneo la Mtongani, Kunduchi jijini Dar es Salaam sehemu ambayo imekumbwa na Janga la Volkano tope katika baadhi ya sehemu na kupelekea madhara kwenye baadhi ya makazi ya Watu.
Askofu Gwajima amefika Kunduchi huku akilakiwa na Wananchi mbalimbali wa eneo hilo ambao hawakumuona tangu kupata ushindi huo sambamba na kupitia sehemu ya Kanisa ambayo pia imekumbwa na Janga hilo la Volkano tope.
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo hayo, Askofu Gwajima amesema kuwa Serikali kupitia Wataalamu wake wameanza kufanyia kazi kwa kufanya uchunguzi wa kina kujua jina la Janga hilo ili kukabiliana nalo.
“Serikali bado inapambana kujua kama hili Janga ni mabadiliko ya tabia nchi, tetemeko la ardhi Au ni aina gani ya janga, lakini kwa mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kawe nawapa pole nyingi kwa janga hili.” amesema Askofu Gwajima.
Askofu Gwajima amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imefika hapo awali kwa lengo la kufanya tathmini kujua idadi ya Wananchi walioathirika na Janga hilo ili kuchukua hatua stahiki kwa Wananchi wote, amesema atafuatilia suala hilo kuhakikisha kila mmoja aliyeathirika anapata haki na stahiki zake ipasavyo.
“Serikali imeanza kutafutia Viwanja Wananchi waliathirika ili wapate pakuishi baada ya janga hili, nitahakikisha wanafanya na kuhakikisha kuwatafutia makazi Wananchi wote na kupatikana kwa vitu vingine vinavyohitajika kwa Binadamu.” ameeleza Askofu Gwajima.
Kwa niaba ya Wananchi wa eneo hilo, Diwani wa Kunduchi, Michael Urio amesema wanashukuru kutembelewa na Mbunge ili kufuatilia janga wanalokabiliana nalo katika kipindi hiki.
Baadhi ya Wakazi wa eneo hilo wameiomba Serikali kuhakikishiwa usalama wao kutokana na athari iliyoikumba eneo wanaloishi, pia wamemuomba Askofu Gwajima kuhakikisha anafuatilia suala hilo.
Kwa mujibu wa Wataalamu, athari ya janga hilo bado haijafahamika ni aina gani na Serikali inaendelea na utafiti wa kina kupata majibu ya haraka na kulishughulikia ili kuhakikisha Wananchi wa maeneo hayo wanaishi kwa amani.
No comments: