AL AHLY SC MABINGWA WA LIGI YA MABINGWA AFRIKA MSIMU WA 2019-2020
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KLABU ya Soka ya Al Ahly ya Misri imeendelea kuweka rekodi katika Soka la Afrika baada ya kutwaa Ubingwa wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) msimu wa 2019-2020 ikiwa ni mara ya tisa kwa ujumla kutwaa Ubingwa wa Michuano hiyo mikubwa barani humo.
Katika mchezo wa Fainali uliopigwa kwenye dimba la Cairo (Cairo International Stadium) nchini Misri, Al Ahly walionyesha nia ya kutwaa ubingwa huo baada ya kutandaza soka safi na la kuvutia ambapo ilipelekea kupata ushindi wa bao 2-1 dhidi ya majirani zao wa Zamalek SC.
Katika dakika ya 5, Al Ahly kupitia kwa Kiungo wake, Amr El Soleya walipata bao la kwanza na la mapema zaidi lakini dakika ya 31 kabla ya mapumziko Zamalek SC walisawazisha bao hilo kupitia kwa Kiungo wao aliyepachika wavuni bao safiiiii, Mahmoud Abderazak Hassan Fadlala (Shikabala) baada ya kuwachambua mabeki wa Al Ahly.
Dakika za lala salama, dakika ya 86 ya mchezo huo wa Fainali, Kiungo Mshambuliaji wa Ahly, Mohamed Magdy aliweka bao safi kwa mtindo wa (Volley) na kuipa timu hiyo Ubingwa wa Michuano hiyo kwa msimu huu wa 2019-2020.
Hadi sasa Al Ahly SC wanaongoza kutwaa ubingwa wa Michuano hiyo ikiwa ni mara ya tisa, wakati Zamalek SC wakiwa wametwaa ubingwa huo mara tano katika historia ya Soka la Afrika kwa ngazi ya vilabu.
No comments: