Ridhiwan ahaidi ushirikiano na DAWASA kuondoa changamoto ya Maji Chalinze
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametembelea ofisi za Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mkoa kazi wa kihuduma Chalinze kwa lengo la kujenga ushirikiano zaidi na kujua mipango iliyopo ya huduma ya maji kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa katika Mji wa Chalinze.
Ridhiwani amebainisha kuwa lengo la ziara yake ni kuishukuru DAWASA kwa kuendelea kutatua changamoto za Majisafi katika jimbo lake na pia kujua mipango ya sasa na ya baadae ya upatikanaji wa Majisafi kwa wananchi wasiofikiwa na huduma hiyo.
"DAWASA ni wadau wakubwa katika kutoa huduma ya majisafi kwa wananchi wa jimbo langu. Hivyo baada ya uchaguzi kuisha nimeona ni vizuri kuwatembelea na kuwasikiliza mipango mbalimbali waliyo nayo na wanayoendelea kuitekeleza katika mji wa Chalinze" alisema Ridhiwani
Ridhiwani alitumia nafasi hiyo kuiomba DAWASA kuharakisha ukamilishaji wa mradi wa Maji wa Mlandizi -Chalinze -Mboga pamoja na mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu kwa haraka zaidi ili wananchi waondokane na kero ya maji .
Kwa upande wake, Meneja wa Dawasa Mkoa wa kihuduma Chalinze, Mhandisi Honest Makoi, ameeleza kuwa huduma ya maji kwa mji wa Chalinze kwa sasa ni nzuri na Mamlaka imepeleka huduma ya maji kwenye vitongoji sita ambavyo havikuwa na huduma.
Amebainisha kuwa kazi iliyofanyika kwenye vitongoji hivyo ni ujenzi wa viosk vya kuchota maji 114 katika Vijiji na vitongoji Visakazi, Mwidu, Gwata, changarikwa kwaruhombo na Kifuleta halmashauri ya Chalinze.
Kazi tunayoendelea nayo kwa sasa ni kufanya marekebisho ya mtandao wa maji tuweze kupeleka huduma ya maji katika Vijiji vya Tukamisasa, Kaloleni na Lulenge. Kazi hiyo inaendelea na wananchi watapata huduma ya maji" alisema Mhandisi Makoi
Ridhiwani aliipongeza Dawasa kwa kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanyika na kuahidi ushirikiano mkubwa baina yao ili dhamira ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani ifanikiwe.
Meneja wa Dawasa Mkoa wa kihuduma Chalinze, Mhandisi Honest Makoi akitoa maelezo kwa Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete mara baada ya kutembelea ofisi za Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mkoa kazi wa kihuduma Chalinze.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Dar es salaam (DAWASA) Mkoa kazi wa kihuduma Chalinze.
No comments: