WANANCHI WANAPASWA KUJITOKEZA KWA WINGI KUPIGA KURA
***********************************
(Na Beatrice Sanga-MAELEZO)
Joto la uchaguzi linaendelea kupanda wakati huu ambapo Tanzania inaelekea kufanya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, ikiwa ni uchaguzi wa sita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995.
Zoezi la kampeni linaelekea ukingoni, huku wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa vikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT-Wazalendo, ADC na CHAUMMA wakizunguka kwa ajili ya kutangaza Ilani na Sera za vyama vyao sambamba na kuomba ridhaa kwa wananchi ili waweze kuchaguliwa katika uchaguzi unaofuata ambapo Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikitumia hazina ya viongozi waandamizi katika kunadi mgombea wa chama hicho,Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika kipindi chote cha kampeni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekuwa ikisimamia ipasavyo shughuli za uchaguzi zikiwemo kuthibitisha wagombea walioteuliwa na vyama vyao, kutoa ratiba za kampeni kwa wakati, kushughulikia rufaa mbalimbali pamoja na kuhakikisha wagombea wote wanafuata kanuni na taratibu za uchaguzi ili kukamilisha zoezi hili kwa hali ya amani na utulivu
Katika kipindi hiki cha kampeni tumeona kiu ya Watanzania katika kushiriki kampeni za uchaguzi, ambapo wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika kampeni za wagombea mbalimbali, hii inaonyesha jinsi gani Watanzania walivyo na hamu ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, japokuwa historia ya ushiriki katika upigaji kura katika mika ya nyuma imeonesha mwamko mdogo sana.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2010 idadi ya wapiga kura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303, lakini waliopiga kura mwaka huo walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 . Mwaka 2015 zaidi ya Watanzania milioni 23 walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, huku Watanzania 15,589,639 pekee ndio waliopiga kura ambayo ni sawa na asilimia 67.34. Hii inaonyesha jinsi gani watu wanavyopuuzia suala la upigaji kura na kupoteza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Tatizo hili la watu kutojitokeza kwa wingi kupiga kura linatokana na kukosa elimu ya uraia na elimu ya mpiga kura. Hivyo wananchi wanahimizwa kuhudhuria na kuzingatia mafunzo ya uraia pamoja na elimu ya mpga kura ambayo hutolewa na asasi za kiraia na NEC ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongizi wanaotaka wawaongoze katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Elimu hii inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi inalenga kuwahamasisha wananchi kutumia kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na kushiriki katika kampeni na kutumia haki yao ya kikatiba ya kikatiba katika kujitokeza na kushiriki kuchagua viongozi watakao waongoza ili kujenga demokrasia na utawala bora nchini.
Kupitia elimu ya mpiga kura, wananchi wananchi wanawezeshwa kuelewa Sheria, Kanuni na Taratibu za mchakato mzima wa uchaguzi, wajibu wao na umuhimu wa wao kushiriki katika uchaguzi. Elimu hii haina hisia, ubaguzi wala itikadi za kisiasa, kidini au kikabila.
NEC, inatumia njia mbalimbali katika kutoa elimu hii kwa wapiga kura hasa kupitia kwenye vyombo vya habari kama vile magazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii. Njia nyingine ambazo wananchi wanapata elimu hii ni kupitia vipeperushi na gari la matangazo ambalo linamilikiwa na Tume. Hivyo kupitia vyombo hivyo wananchi wanapata taarifa muhimu kuhusu uchaguzi kuanzia hatua ya kwanza ya kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hadi hatua ya mwisho ambayo ni siku ya kupiga kura. Wananchi wanafahamishwa kuhusu kituo cha kupiga kura, muda wa kupiga kura, tarehe ya kupiga kura na matarajio ya mpiga kura anapofika kituoni na namna ya kupata matokeo ya uchaguzi.
Pamoja na NEC, kutoa elimu ya mpiga kura, wananchi pia wanapata elimu ya uraia ambayo inahusu haki na wajibu wa raia katika Nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Elimu hii ina sifa ya kumjengea uwezo mwananchi kujitambua na kuzijua haki zake zinazomwezesha kufanya maamuzi sahihi katika mambo yanayomzunguka, kama vile katika masuala ya uchaguzi ambapo inamfanya mwananchi ajue umuhimu way eye kushiriki katika mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na kujua taratibu anazotakiwa kufuata anapokuwa katika kituo cha kupiga kura.
Aidha, wapiga kura wanapaswa kuwa tayari kwa hiyari yao na kwa ufahamu wao na kwa kujiamini kwao kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura wakiwa na mtazamo wa kukuza demokrasia.
Zikiwa zimebaki siku chache kufikia siku ya kupiga kura hapo tarehe 28, Oktoba, Watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kutimiza haki yao ya msingi na ya kikatiba ili waweze kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo kwao na kwa taifa zima kwa ujumla.
Wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura bila kuwa na wasiwasi wala hofu kwani, upigaji kura upo kisheria, chini ya kanuni ya 3.1 (b) ya maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015. Serikali imepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa kunakuwapo hali ya usalama, amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Kutokana na kupata elimu ya kutosha kuhusu masuala ya uchaguzi, wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura kama vile wanavyojitokeza katika kampeni, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza haki yao ya kikatiba katika kutekeleza demokrasia.
No comments: