SHIVYAWATA MANYARA WAIPONGEZA TUME YA UCHAGUZI




Mratibu wa uchaguzi wa Mkoa wa Manyara, Kennedy Kaganda akizungumza na waelimishaji jamii wa Mkoa huo wanaotoa elimu ya mpiga kura kwenye halmashauri saba za wilaya za mkoa huo.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation CSP Nemency Iriya akizungumza kwenye mafunzo ya elimu ya uchaguzi kwa waelimishaji jamii wa Mkoa wa Manyara wanaotoa elimu kwa makundi mbalimbali Mkoani Manyara.

Waelimishaji jamii wa Mkoa wa Manyara wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kupatiwa mafunzo ya elimu ya uchaguzi kwa makundi maalumu ya walemavu, wanawake na vijana.
……………………………………………………………………………….
Katibu wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Shivyawata Mkoani Manyara, Peter Sanka ameipongeza Tume ya Taifa ya uchaguzi kwa kuandaa utaratibu mzuri wa makundi maalumu hasa walemavu kushiriki kwenye mazingira rafiki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. 


Sanka ameyasema hayo mjini Babati, wakati akizungumza kwenye mafunzo ya elimu ya uchaguzi kwa makundi maalumu ya walemavu, wanawake na vijana, yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation (CSP). Ameishukuru Tume ya uchaguzi kwa kuandaa mazingira rafiki wakati wa kupiga kura na kusema ili kukuza ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye uchaguzi, wanapaswa kufahamu utaratibu uliowekwa kwenye kituo cha kupigia kura. 


Amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kufahamu utaratibu wa uwepo wa vifaa vya uchaguzi vyenye nukta nundu kwenye kila kituo cha kupiga kura. Amesema uwepo wa kituturi kinachomwezesha mlemavu wa viungo kupiga kura kwenye kituo hivyo anatakiwa kupewa msimamizi. 


“Watu wenye ulemavu watapewa kipaumbele wafikapo kituoni, wanaruhusiwa kwenda na wasaidizi wao na haki na wajibu wao kushiriki kwenye uchaguzi,” amesema Sanka. Mkurugenzi wa shirika la CSP Nemency Iriya amesema ili kukuza ushiriki wa wanawake kwenye uchaguzi, wanapaswa kufahamu utaratibu kuwa wana haki ya kupiga kura kama ile haki ya kujiandikisha. 


Iriya amesema kipaumbele kitatolewa kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha na uhuru wa kushiriki mikutano ya kampeni. “Kutoa mawazo yao na kusikilizwa kwenye mikutano ya kampeni na wanatakiwa kumchagua mgombea wanayemtaka na siyo kwa shinikizo la mtu yeyote,” amesema.
Mwanasheria wa CSP Eliakim Paulo amesema ili kukuza ushiriki wa vijana wanatakiwa kujua wana uhuru wa kushiriki mikutano ya kampeni. 


Eliakim amesema vijana watakaopiga kura kwa mara ya kwanza wanatakiwa kujua kuwa wana haki ya kupiga kura kama walivyojiandikisha. Amesema wanapaswa kutoa mawazo, maoni na kusikilizwa na kumchagua mgombea wanaomtaka bila kulazimishwa na mtu yeyote. “Kwa wanaopiga kura kwa mara ya kwanza wana haki ya kuulizia kwa msimamizi wa kituo jambo lolote ambalo hawalifahamu juu ya kupiga kura na wanatakiwa kujibiwa,” amesema.

No comments: