JAJI KIONGOZI ATAKA MASHAURI YA MIRATHI YA MUDA MREFU KUMALIZIKA MWAKA HUU
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu za Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu za Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na watumishi wa Mahakama za wilaya ya Magu alipofanya ziara kukagua shughuli za Mahakama katika kanda ya Mwanza. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika na wengine ni viongozi wa Mahakama kutoka Makao Makuu ya Mahakama Kuu
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu za Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika
************************************
Na Lydia Churi- Mahakama, Mwanza
Jaji Kingozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na Mahakimu wote kuhakikisha wanasikiliza mashauri yanayohusu Mirathi yaliyofunguliwa muda mrefu na kuyamaliza ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza katika siku ya kwanza ya ziara yake kwenye kanda hiyo, Jaji Kiongozi amesema mashauri hayo ya mirathi yaliyofunguliwa muda uliopita hayapaswi kuvuka mwaka 2020 na amesisitiza kuwa ikiwezekana yasikilizwe hata siku ya Jumamosi ili kuhakikisha yanamaliza ndani ya mwaka huu.
“Mashauri ya Mirathi nyuma yake kuna wajane, wagane na Watoto yatima ambao wanahitaji matunzo ikiwemo kupata haki yao ya kusoma shule, ziko familia zinazovurugika na watoto kupata shida kutokana na mashauri ya aina hii kuchelewa kumalizika”, alisisitiza Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi pia amewataka Majaji na Mahakimu waliopangiwa kusikiliza mashauri ya mirathi kujiwekea mikakati itakayowezesha mashauri hayo kumalizika ndani ya muda uliopangwa. Aliongeza kuwa viongozi hao hawatapaswa kuchukua likizo mpaka pale watakapokuwa wamemaliza kusikiliza mashauri waliopangiwa.
Wakati huo huo, Jaji Kiongozi amewashauri watumishi wa Mahakama kujiendeleza kielimu ili kuendana na wakati. Akitolea mfano wa kada ya Mahakimu, Dkt. Feleshi amesema hivi sasa Mahakimu wanaoomba ajira, asilimia kubwa wanakuwa tayari wameshajiendeleza kielimu na kuwa na sifa nyingi za kitaaluma walizozipata kipindi walipokuwa wakisubiri kupata ajira.
Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Ilemela alipoenda kumtembelea Kiongozi huyo, Jaji Kiongozi amewaomba Maafisa Tarafa nchini kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha upatikanaji wa haki zao.
“Maafisa Tarafa kama walinzi wa amani mnao wajibu wa kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuwa Mahakama inaondokana na ulazima wa wananchi kufika mahakamani kufungua mashauri na badala yake watumie Tehama ili kurahisisha upatikanaji wa haki,” alisema.
Alisema faida za kutumia mfumo wa Tehama katika kurahisisha upatikanaji wa haki ni pamoja na kuondokana na matatizo ya rushwa na kupunguza muda wa wananchi kufika mahakamani ili muda huo wautumie kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Akizungumzia changamoto za huduma ya Posta Mlangoni ambayo pia hutumika kurahisisha upatikanaji wa nyaraka mbalimbali za kimahakama ikiwemo nakala za hukumu kwa wananchi waliokuwa na shauri mahakamani, Jaji Kiongozi amewataka wananchi wanaobadilisha anuani zao kuijulisha Mahakama ili waweze kupelekewa nakala zao za hukumu kupitia huduma hiyo ya Posta Mlangoni.
Posta Mlangoni ni huduma iliyoanzishwa na Mahakama ya Tanzania baada ya kuingia mkataba na Shirika la Posta Tanzania uliowezesha shirika hilo kusambaza nyaraka mbalimbali za kimahakama katika maeneo yote nchini.
Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi amewataka Majaji na Mahakimu wa kanda ya Mwanza kuyamaliza mashauri yote ya kanda ya Musoma yaliyosajiliwa kwenye kanda ya Mwanza kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama kuu kanda ya Musoma ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Jaji Kiongozi anaendelea na ziara katika kanda ya Mwanzo ambapo anatarajiwa kukagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Ukerewe, Kwimba, Chato, Bukombe pamoja na Mkoa wa Geita.
No comments: