MILIONI 56 ZA TUMIKA KUKARABATI MAGARI YA POLISI RUVUMA

Na Muhidin Amri, Songea
KAMPUNI ya Usafirishaji ya Super Feo &Selou Express ya mkoani Ruvuma,imekarabati magari 10 ya polisi ikiwemo lori moja lililakaa kwa zaidi ya miaka mitano bila kufanya kazi kwa gharama ya shilingi milioni 56.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Kisiwa Abrahabi amesema, Super Feo imekarabati magari hayo kama sehemu ya mchango wake kwa jeshi hilo ili kuwaongezea uwezo katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku ikiwemo suala la ulinzi wa raia na mali zao ili kuhakikisha mkoa wa Ruvuma unaendelea kuwa kisiwa cha Amani na utulivu wakati wote.

Kisiwa alisema, kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Polisi na taasisi nyingine za Serikali mkoani Ruvuma kwa lengo la kuboresha huduma zinazotoa kwa wananchi ili kurahisisha utendaji wake ili kuharakisha maendeleo kwa nchi na Watanzania kwa jumla.

Aidha, amewataka wafanya biashara wengine kujitokeza kulisaidia jeshi la Polisi kwani ana amini kwamba bado lina uhitaji wa vitu vingi ikiwemo vitendea kazi ambavyo vitaliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake ya kila siku hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani hapa kamishina msaidizi wa Polisi Simon Maigwa mbali na kuishukuru kampuni ya Super Feo&Selou Express kwa msaada huo alisema, magari hayo yatatumika kuimarisha utendaji wa majukumu ya Askari na maafisa wa jeshi hilo.

Kwa mujibu wa Maigwa ni kwamba,ukarabati wa magari hayo ni ishara kwamba wadau wanaridhika na utendaji wa jeshi la polisi katika kusimamia haki na rasilimali zao na kusisitiza kwamba ni wajibu wa kila mdau kulisaidia jeshi hilo katika nyanja mbalimbali.

Alisema, kati ya magari hayo Toyota Landcruser 6 malori 3 na gari moja la washawasha ambao linatumika kutawanya watu pale wanapokuwa katika mikusanyo isio rasmi au kwenye vurugu.

Kamanda Maigwa alisema, magari hayo yatapelekwa katika vikosi mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha utendaji wake kwani licha ya askari kuwa na moyo wa uzalendo,lakini wakati mwingine waloshindwa kufikia malengo kutokana na uhaba wa vitendea kazi.

Aidha alisema, katika kipindi cha miaka mitano jeshi la polisi mkoa wa Ruvuma limefanikiwa kupunguza ajali za barabarani kutoka 2440 mwaka 2011- 2016 hadi kufikia ajali 692 mwaka 2020 ikiwa ni tofauti ya ajali 1752 sawa na asilimia 71.81.

Kamanda Maigwa alisema, katika kipindi cha awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuri, jeshi hilo limefanikiwa kukusanya kiasi cha bilioni 5,591,130.000 sawa asilimia 208.4 ikiwa ni ongezeko la bilioni 3,777,930.000 ikilinganisha na makusanyo ya shilingi bilioni 1,813,200.000 ya mwaka 2011-2016.

Katika hatua nyingine kamanda huyo wa Polisi alisema, ofisi yake imepokea jumla ya shilingi milioni 12 kutoka kwa Mkuu wa Jeshi hilo Nchini ambazo zimetumika kununulia matairi ya magari ambayo yamegawiwa kwa wakuu wa polisi wilaya na vikosi vyote vya mkoa wa Ruvuma.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea wamelipongeza jeshi la Polisi mkoa wa Ruvuma kutokana na kazi nzuri ya kupunguza matukio ya uharifu na ujambazi katika mkoa huo pamoja na ajali na vifo vya barabarani.

Hata hivyo,wameiomba Serikali kuboresha makazi,maslahi ya polisi na kuwapa vitendea kazi ili kazi za ulinzi wa raia na mali zao zifanyike kwa weledi mkubwa.

No comments: