DITOPILE AZINDUA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA KIBAIGWA
Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akizungumza katika mkutano wa kampeni za Udiwani Kata ya Kibaigwa.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za kata ya kibaigwa, Mariam Ditopile (kulia) akimnadi Mgombea Udiwani wa kata hiyo, Chande Mrisho.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za Udiwani kupitia CCM kata ya Kibaigwa mkoani Dodoma, Mariam Ditopile akiinadi Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa wananchi.
* Asema Dkt. Magufuli amewainua Wamachinga.
Na Charles James, Michuzi TV
KAMATI ya siasa CCM mkoa wa Dodoma, imezindua rasmi kampeni zake ngazi ya kata nafasi ya udiwani katika jimbo la Kongwa kata ya Kibaigwa.
Kampeni hizo zimefunguliwa katika viwanja vya soko la mbogamboga Kibaigwa, ambapo wajumbe mbalimbali walihudhuria ufunguzi wa kampeni hizo ngazi ya kata nafasi ya udiwani katika kuhakikisha wanatimiza jambo kuu la kuomba kura kwa wananchi lengo likiwa kuomba ridhaa ya kuitumikia serikali ya jamhuri ya muungano kwa awamu ya pili kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2020 mpaka 2025.
Awali akizungumza kwenye ufunguzi huo, Mgombea Ubunge nafasi ya viti maalumu UWT Mariam Ditopile amesema ufunguzi huo ni sehemu ya kueleza yale yaliyoahidiwa mwaka 2015 wakati serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani.
“ Kurudi kusema nini tumefanya, kipi kimekamilika, kipi kipo kwenye mchakato na nini tunategemea kufanya kumalizia yale na kuanza mengine mapya ndiyo maana kauli mbiu yetu mwaka huu sisi kama CCM tunasema’ tumeahidi, tumetekeleza kwa kishindo! tunataka mtuchague tena ili kazi iendelee," Amesema Ditopile.
Aidha Ditopile amesema kuwa serikali ya awamu ya tano imejipambanua Zaidi kwani imeweza kuinua sana watu wa hali ya chini ikiwemo mama lishe, wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kutoa vitambulisho ambavyo vimeweza kuwasaidia katika kufanya biashara zao bila budha na kufanikisha suala zima la kuwainua kiuchumi.
Pamoja na hayo amesema kuwa serikali ya awamu ya tano imefanya mambo kadha wa kadha katika kuhakikisha inatimiza mambo yote iliyoahidi wakati inaomba ridhaa ya kuingia madarakani ikiwa ni Pamoja na kufanya kazi kwa bidii kuanzia ngazi ya serikali za mitaa mpaka uongozi wa juu.
Amesema hakuna eneo ambalo halijaguswa ambapo sekta ya Afya, Elimu, Miundombinu na utendaji umekuwa wenye weledi na hivyo kuwataka wananchi wa Kibaigwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwa awamu ya pili ikiwa ni Pamoja na kuchagua wagombea wote wa nafasi mbalimbali kuanzia nafasi ya udiwani, ubunge na Rais ili waweze kumsaidia Rais katika kutimiza yale yote yaliyo kwenye Ilani mpya ya CCM ya 2020.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Kibaigwa jimbo la Kongwa, Chande Mrisho aliwaomba wananchi wampee ridhaa ya kuwatumikia ili aweze kuyamalizia yale yalioachwa na mgombea aliyemaliza mda wake kwani kata hiyo imekua na changamoto mbalimbali hapo awali hivyo kama wananchi wa Kibaigwa wajitoe kimaso maso kwa kumpigia kura za kumwagikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Pamoja na wagombea wote wa CCM.
No comments: