DK.JOHN MAGUFULI ASEMA ATACHANGIA SH.MILIONI 10 KUKAMILISHA UJENZI KITUO CHA AFYA KAZURAMIMBA

 

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kazuramimba

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli ameahidi kuchangia Sh.milioni 10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha afya Kazuramimba mkoani Kigoma baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.

Kituo hicho ambacho Dk.Magufuli ameahidi kutoa kiasi hicho cha fedha ni baada ya kufurahishwa na jitihada za wananchi wa Kazuramimba kuanza ujenzi wa kituo hicho kwa nguvu zao, hivyo baada ya kumalizika uchaguzi Mkuu Oktoba 28 ,2020 ndani ya miezi mitatu kitakuwa kimekamilika.

Akizungumza na wananchi hao leo Septemba 20, mwaka 2020, Dk.Magufuli amesema kwamba lazima kituo hicho kimalizike ujenzi wake,hivyo atakapochaguliwa na kushinda urais atatoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kukamilisha kituo hicho.

"Najua nitashinda Urais , hivyo katika kipindi cha miezi mitatu tutakuwa tumekamilisha ujenzi.Hiki ni kipindi cha kampeni hivyo nikitoa hizi hela ambazo nataka kuchangia watasema natoa rushwa,ndio maana nasema nitatoa baada uchaguzi kwisha.

"Wananchi wa Kazuramimba umeonesha mfano mzuri sana kwa kuamua kuanza ujenzi kwa nguvu zenu, na wanasema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.Nami niwaahidi wananchi wa hapa nitachangia ujenzi wa kituo hiki cha afya,"amesema Dk.Magufuli.

Hata hivyo amesema mbali ya kukamilisha ujenzi, atapeleka dawa na vifaa tiba pamoja na watalaam ili kituo kianze kutoa huduma za matibabu na kwamba kiwe kinatoa na huduma za upasuaji."Tunataka hiki kituo cha afya kiwe kinafanya na operesheni."

Dk.Magufuli amesema kutokana na umuhimu wa kituo hicho, Waziri wa Afya ambaye atamteua kazi yake ya kwanza itakuwa ni kushughulikia kituo hicho ili kianze kazi ya kutoa huduma kwa wananchi hao.

Wakati huo huo Dk.Magufuli ameendelea kuzungumzia mkakati uliopo wa kuboresha miundombinu ya barabara ambapo amesema anataka mtu atoke Kazuramimba hadi Dar es Salaam na Kazuramimba hadi Tunduma bila kukanyaga changarawe.

Hata hivyo amewaambia wananchi hao kuwa miaka mitano aliwaomba kura na walimchagua yeye, mbunge na madiwani wa CCM na katika kipindi chote hicho wamefanya waliyoweza na wataendelea kutekeleza mengine yaliyobakia kwani maendeleo ni changamoto na changamoto zinatatuliwa moja baada ya nyingine.

"Wakati tuaomba kura hapa Kazuramimba hata umeme ulikuwa hakuna, leo upo.Hakukuwa na majengo lakini leo majengo yameongezeka na hata idadi ya watu imekuwa kubwa.Kazuramimba kuna wakazi zaidi ya 65000, mji ni mkubwa, mengine niachieni mimi.

"Naomba mniamini,mnipe kura, najua katika mikakati ya kugombea ndani ya CCM walikuwepo wagombea wengi, hata aliyekuwa mbunge wa hapa naye alikuwepo wakati wa mchakato wa kura za maoni na yuko hapa leo ameniombea kura mimi,amemuombea kura mgombea ubunge Nashon, amewaombea kura madiwani wetu wa CCM,"amesema.

No comments: