WANASIASA NCHINI WAOMBWA KUJIEPUSHA NA KAULI ZINAZOASHIRIA KUHATARISHA AMANI YA NCHI
Na Mwandishi Wetu
TAASIS Habari Development Association imesema imestushwa na matamshi yanayoendelea kutolewa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wakiwemo baadhi ya wagombea nafasi ya urais, ubunge na udiwani ambayo yanahatarisha amani ya nchi yetu hususani kwenye kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo na Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo Bernard James kwa niaba ya viongozi wenzake amesema ni vema wanasiasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wakiwemo wagombea urais , kuchunga ndimi zao, waache kutoa maneno ya uchochezi ya kuwagawa watanzania.
"Kwa mfano mgombea urais wa CHADEMA Tundu Lissu alipokuwa akihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa Chama hicho ambao ulimpitisha kuwa mgombea uliofanyika Agosti mwaka huu jijini Dar es salaam, alinukuliwa akisema “uhuni sasa basi” .
"Pia amenukuliwa kwenye mikutano yake wakati akizunguka mikoani akitafuta wadhamini akisema kuwa akishindwa uchaguzi atahamasisha wafuasi wake na wananchi waingie barabarani.Aidha mara kadhaa akihamasisha wagombea wachukue na kurudisha fomu kwa maandamano na kutishia kwamba maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wasipokuwepo Ofisini, Ofisi zao zitakuwa halali yao. Huyu ni mgombea ambaye amekuwa akitoa matamshi hayo kwenye mikutano yake mbalimbali,"amesema wakati akisoma tamko lao la kuhamasisha amani na utulivu .
Aidha amesema kuna mgombea mwingine wa urais upande wa Zanzibar anayewakilisha Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Ahmad amekuwa akitoa matamshi kuwa safari hii hatakubali kushindwa tena na anahamasisha wapiga kura kulinda kura kwa silaha za jajadi.
"Pia anadai kuwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni matawi ya CCM, kitu ambacho sio kweli.Ipo mifano mingi ya viongozi hasa wa upinzani ambao wamekuwa matamshi ambayo hayana muelekeo mzuri.
"Kwa hata kauli ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyoitoa hivi karibuni jijini Dar es Salaam akidai kuna wagombea ubunge wa chama chake wametekwa na kuteswa na utekaji huo ni wa kisiasa na unafanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
"Ushauri wetu kwa kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo ni kuwa angesubiri vyombo vinavyofanya uchunguzi wa jambo hilo vikamilishe kazi yake.Kauli hiyo ya Zitto inaweza kuibua chuki baina ya wanachama wa vyama vya siasa na hivyo kuleta vurugu hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu"amesema.
James amesema.
Kupitia tamko hilo, James amesisitiza kauli hizo ni za hatari na zinahatarisha amani ,utulivu na umoja wa Taifa letu uliojengwa na waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Amri Abeid Karume
Aidha wamekuwa wakishuhudia matamshi ya shari yakitolewa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA akiwemo mgombea wa ubunge Jimbo la Iringa Mjini, Peter Msigwa katika mikutano yake ya hivi karibuni kwani matamshi mengi yaliyotolewa hayakuwa ya staha.
"Tunawasihi wagombea hao kuzingatia sheria za nchi yetu wakati wote wa kampeni na baada ya matokeo kutangazwa na hivyo waache kutoa kauli za shari vinginevyo nchi yetu inaweza kuingia kwenye machafuko na vurugu kama ilivyowahi kutokea kwenye nchi za jirani.
"Tunawauliza wanasiasa wetu je, wanapenda yaliyotokea huko yatokee nchini mwetu? Ni dhahiri hali kama hiyo inapotokea waathirika ni wananchi, hususani akina mama, wazee na watoto.
"Tunatoa mwito kwa wananchi pamoja na wanachama wa vyama vyote vya siasa kupuuza kauli hizo zinazotolewa na baadhi ya wagombea ili kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu kwa sababu machafuko yakitokea wao ndio watakao athirika,"amesisitiza.
Wakati huo huo taasisi hiyo imewashauri waliokuwa wagombea katika hatua ya awali ya uchaguzi ndani ya CCM ambao hawakufanikiwa kupitishwa na vikao vya chama hicho kuwa wawe na subira.
No comments: