Wananchi washauriwa kujijengea tabia ya kusaidia watu wenye uhitaji.
Jane Edward,Arusha.
Wananchi wameshauriwa kuwa na tabia ya kupenda kujitolea kwa kuwasaidia watu wenye uhitaji hususani makundi maalumu ili waweze kuondokana na changamoto mbalimbali za kimaisha zinazowakabili.
Hayo yalisemwa Jana na Mkuu wa wilaya ya Arumeru ,Jerry Muro wakati akizungumza na wananchi katika hafla maalumu ya kumkabithi nyumba Bibi kikongwe Eliakunda Mafie (70 ) baada ya kujengewa nyumba hiyo na waumini wa huduma ya mbingu duniani iliyopo Ngulelo mjini hapa.
Muro alisema kuwa,kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye makundi maalumu hususani wazee kwani wengi wao wamekuwa hawana msaada wowote na kuishi katika mazingira magumu ,Jambo ambalo Kila mmoja wetu anatakiwa kutimiza wajibu wake kwa kuwasaidia.
"Kwa kweli hiki kilichofanywa na waumini wa huduma hii ambao wameweza kujinyima na kutoa chochote katika kuhakikisha Bibi huyu anajengewa nyumba na kuishi katika mazingira mazuri kimeugusa moyo wangu Sana na kamwe Mungu hatawapungukia kwa hiki mlichokifanya kwani hakijawahi kufanywa na mtu yoyote.'alisema Muro.
Aidha alisema kuwa, kumekuwepo na watu wengi wenye uwezo mkubwa wa kufanya mambo Kama hayo lakini hakuna hata mmoja amewahi kuwaza kufanya Jambo kubwa Kama hilo,hivyo huo ni mfano wa kuigwa na wananchi pamoja hata na huduma mbalimbali .
Naye Mtumishi Mwalimu wa huduma hiyo ya Mbingu duniani,Onesmo Nnko alisema kuwa,katika huduma hiyo wamekuwa wakiguswa kusaidia watu wenye mahitaji maalumu hususani wazee ambapo hiyo ni mara ya pili kujenga nyumba Kama hiyo kwa wazee.
Mwalimu Onesmo alisema kuwa,wamekuwa wakiangalia watu wenye uhitaji maalumu hususani wazee na kuweza kujinyima na kuchanga chochote walichonacho Kama sadaka ya kuwajengea nyumba na kuweza kuondokana na mazingira magumu waliyokuwa wakiishi hapo awali .
"Kwa kweli huduma yetu tumekuwa tukifanya maswala mbalimbali ya utoaji kwa njia tofauti kwani sadaka ipo kwa njia nyingi Sana ,sisi tumeona sadaka yetu tuelekeze kuwajengea makazi mazuri wazee ambao wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na hiyo ni nyumba ya pili tunakabithi kwa mwezi huu na zoezi hili ni endelevu."alisema Mwalimu Onesmo.
Alisema kuwa,nyumba ya kwanza ambayo nayo wamekabithi hivi karibuni walimjengea mzee Petro Akyoo (81) mkazi wa kata ya Bangata ambayo iligharimu kiasi cha shs 5 milioni, huku nyumba ya pili ya Bibi huyo ikigharimu kiasi cha shs 6.5 milioni na kuwa wanaendelea na utaratibu huo lengo ni kuhakikisha wanagusa maisha ya watu wenye uhitaji maalumu kwa njia tofauti.
"Tumeona serikali ikifanya mambo mengi tena makubwa ya maendeleo ambayo kila mmoja anayaona ,hivyo kwa upande wetu na sisi tukaona ni vyema tukaiunga serikali mkono kwa kusaidia watu wenye mahitaji maalumu ili waweze kuondokana na mazingira wanayoishi'alisema Mwalimu Onesmo.
Naye Kikongwe huyo, akizungumza baada ya kukabithiwa nyumba hiyo alimshukuru Mungu kwa kumletea watu wenye moyo wa kipekee ambao wameweza kumkumbuka na kumjengea nyumba kutokana na hali ngumu ya maisha aliyokuwa akiishi.
Alisema kuwa,jambo hilo kwake ni historia katika maisha yake na kamwe Mungu hatawapungukia na kuwaomba kuendelea kuwasaidia wazee wengine wenye mahitaji Kama hayo kwani ni kundi ambalo limesahaulika Sana katika jamii.
No comments: