OLE SENDEKA (SIMBA WA MANYARA) APOKEWA KWA SHANGWE AKIENDA KUCHUKUWA FOMU YA UBUNGE

Mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) akiwapungia mkono ili kuwasalimia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipofika kuchukua fomu ya kuomba kuteulia kugombea ubunge.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka (kulia) akisindikizwa na wanachama wa CCM alipofika kuchukua fomu ya kuomba kuteulia kugombea ubunge kwenye ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo, nyuma yake ni Katibu wa CCM wa wilaya hiyo Ally Kidunda.
Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Simanjiro Yefred Myenzi (kushoto) akimkabidhi fomu za kuomba uteuzi wa kugombea ubunge wa jimbo hilo Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) kwa ajili ya kuwakilisha CCM kwenye uchaguzi huo, kulia ni waliokuwa watia nia Nai Tukay na Kiria Laizer.

Na Mwandishi wetu, Simanjiro

CHRISTOPHER Ole Sendeka (Simba wa Manyara) aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Simanjiro kwa miaka 10 mfululizo kutoka maka 2005/2015 ambaye alishinda kura ya maoni hivi karibuni na jina lake kurudisha na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, amechukuwa fomu ya kugombea ubunge huo huku akisindikizwa na maelfu ya wanachama wa chama hicho.

Ole Sendeka huku akiwa na msafara wa magari na pikipiki amepokelewa kwa maandamano na kuahidi kuwatumikia wananchi wa eneo kwa uaminifu na uadilifu endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Orkesumet baada ya kuchukuwa fomu amesema anatambua wananchi wa eneo hilo wana kiu kubwa ya kupatiwa maendeleo hivyo atajitahidi kuhakikisha anatimiza suala hilo.

Amesema muda wa kampeni ukifika atazungumza maendeleo yote wananchi wanayotarajia ikiwemo barabara ya lami ya Kia-Mirerani-Orkesumet  na kukamilishwa kwa mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Orkesumet.

“Nawashukuru sana kwa ninyi kunisindikiza kuchukua fomu kwani mmekuja kwa wingi na nawashukuru sana ila wote tuwe mabalozi wazuri wa Rais John Magufuli kuhakikisha anachagulia kwa kura nyingi za kishindo,” amesema Ole Sendeka.

Mwanachama wa CCM wa kata ya Terrat, Baraka Mollel aliishukuru NEC kwa kurudisha jina la Ole Sendeka ambaye wajumbe wa CCM wa wilaya ya Simanjiro walimchagua kwa kura 306 hivyo kushika nafasi ya kwanza.

“Tunamshukuru Rais Magufuli kuturudishia Simba wa Manyara kwani wananchi wa Simanjiro bado wanampenda na wanahitaji kutumikiwa na Ole Sendeka katika kipindi kingine cha miaka mitano,” amesema Mollel.

Hata hivyo, Katibu wa CCM wilaya ya Simanjiro, Ally Kidunda amewataka wanachama wote wa CCM waliochukua fomu za kugombea na majina yao kutorudi wavunje makundi na kumuuza mgombea mmoja wa CCM aliyeteuliwa.

“Pamoja na hayo nawasihi wanachama wa CCM acheni tabia za kuzodoana na kutoleana maneno ya kashfa kwa wale alioshinda na kushindwa kwani hivi sasa tunatetea chama chetu siyo mtu,” amesema Kidunda.

Kwa upande wake, msimamizi wa uchaguzi huo, Yefred Myenzi amesema hadi hivi sasa wagombea wawili Ole Sendeka wa CCM na Emmanuel Landey ndiyo wanachama wa vyama vya siasa waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.

Myenzi amesema atashirikiana na maofisa watano wa ofisi yake katika kuhakikisha shughuli ya uchaguzi mkuu unafanyika kwa haki na kufuata kanuni, taratibu na sheria za uchaguzi zilizoeka kikatiba kupitiaTume ya Taifa ya uchaguzi.

No comments: