ESTL YAWAKUTANISHA WADAU KUJADILI UUNDAJI KAMATI ZA KUPINGA MATUKIO YA UKATILI
Mtendaji Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL), Joshua Ntandu, akizungumza katika kikao kilicho wakutanisha wadau mbalimbali wa Kata ya Kinyagigi katika Wilaya ya Singida Vijijini kwa ajili ya kuunda kamati za vijiji za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia mwishoni mwa wiki. Kutoka kulia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Veronika Mure na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kinyagigi, Nives Mapunda.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Veronika Mure, akizungumzia majukumu ya Mtakuwwa.
Wadau wakipitia mwongozo wa Mtakuwwa.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kinyagigi, Nives Mapunda, (katikati) akizungumza katika kikao hicho.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kinyagigi, Hamisi Mohamed, akizungumza katika kikao hicho.
Mwakilishi wa vijana wa kata hiyo, Alfred Mohamed, akizungumza kwenye kikao hicho.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mitula, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Majadiliano yakifanyika.
Kiongozi wa Dini ya Kikristo, Emanuely Ng'eni, akizungumza kwenye kikao hicho.
Mmoja wa Wajumbe wa kikao hicho, Jackline Alute akizungumza.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL)limewakutanisha wadau mbalimbali wa Kata ya Kinyagigi katika Wilaya ya Singida Vijijini kwa ajili ya kuunda kamati za vijiji za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Wadau waliokutanishwa na shirika hilo ili kupata mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuunda kamati hiyo ni wakunga wa jadi, walimu wa afya mashuleni, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, waganga wa tiba asilia, mangariba na watu wenye mahitaji maalumu.
Kikao hicho kilicho keti mwishoni mwa wiki katika kata hiyo kililenga kuunda kamati za vijiji zitakazokuwa zikifuatilia vitendo vya ukatili katika wilaya hiyo pamoja na kupitia mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA 2017/18 hadi 2021/22.
Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Joshua Ntandu alisema shughuli hiyo inafanyika kwa ufadhili wa Ubalozi wa Finland Dar es Salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Singida vijijini kwa kutekeleza mradi huo katika Kata tano ambazo ni Maghojoa, Mwasauya, Merya, Munghunga na Kinyagigi.
Alisema shughuli ambazo kamati hiyo itazifanya kwa kushirikiana na shirika hilo ni kukutana na kina mama wanaohudhuria kliniki na kuwapa mafunzo, kutoa mafunzo kwa viongozi wa dini, vijana walio nje ya shule,wanafunzi mashuleni na kuimarisha klabu za wanafunzi (KLABU JUU)
Alitaja shughuli nyingine ni kuandaa midahalo ya wazi ya kujadili namna ya kutokomeza mila potofu na kufanya mikutano ya hadhara.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Veronika Mure alisema majukumu ya kamati hiyo nikuhakikisha utekelezaji wa mpango kazi huo na shughuli za hutoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi unaendana na mikataba ya Kikanda na Kimataifa ya haki na ustawi wa Wanawake na Watoto pamoja na Sera, Sheria na Miongozo ya Serikali.
Washiriki wa kikao hicho walisema vitendo vya ukeketaji na matukio ya ukatili wa kijinsia bado ni changamoto na kwamba maovu hayo hufanyika kwa siri kubwa.
“Matukio ya vitendo vya ukeketaji na ukatili wa kijinsia bado vinafanyika na kibaya zaidi watuhumiwa wakikamatwa na kufikishwa polisi au mahakamani huachiwa hivyo kuleta sintofahamu miongoni mwa jamii" alisema mmoja wa wajumbe hao Jackline Alute.
Alute alisema suala la ukeketaji, mimba na ndoa za umri mdogo yamekuwa ni matukio ya kawaida na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa hata baada ya kumbaini mtuhumiwa walalamikaji na ndugu wa mtuhumiwa hukutana na kuyamaliza kiaina.
Katika kikao hicho wajumbe hao walijifunza mbinu za kuibua vitendo vya ukatili wa kijinsia na jinsi ya utoaji wa taarifa kwa vyombo husika kwa kushirikiana na ESTL.
Washiriki hao walipata fursa ya kukaa katika makundi na kutengeneza mpango kazi utakaowaongoza katika kutekeleza majukumu yao dhidi ya vita ya matukio ya ukatili wa kijinsia na ukeketaji ambapo kila baada ya miezi mitatu watakuwa wakifanya kikao cha tathmini.
“Lengo la mpango kazi wetu huu ni kutusaidia kuanza kuibua matukio yote ya ukatili, kuhamasisha jamii kuacha kufanya vitendo hivyo na kufanya ufuatiliaji na hatimaye kutoa taarifa kwa MTAKUWWA na kwenye mfumo wa Tehama uliobuniwa na ESTL ili kutoa taarifa za matukio ya ukatili kwa kutumia namba 0710567003, “ alisema Alfred Mohamed.
No comments: