Wananchi washauriwa kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara na kuwa na bima aa afya ambayo itawasaidia pindi watakapouguwa
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
30/07/2020 Wananchi wameshauriwa kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara kwa kufanya hivyo watatambua kama wana maradhi au la na kama wana maradhi wataweza kupata huduma za matibabu kwa wakati.
Pia wameombwa kuwa na bima ya afya ambazo zitawasaidia kupata matibabu pindi watakapouguwa kwani maradhi huja muda wowote, wakati wowote na mahala popote bila ya kupiga hodi.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na aliyekuwa Mbunge wa Nzega Mhe. Lucas Lumambo Selelii aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza kwa furaha na mwandishi wa habari hii Mhe. Selelii alisema huduma za matibabu ya moyo ya kibingwa ambayo hapo awali yalikuwa yakipatikana nje ya nchi sasa yanapatikana hapa nchini kwa kiwango cha juu kupitia madaktari wabobezi na wataalam wa upasuaji wa moyo.
“Matibabu niliyoyapata pamoja na mengine yanatotolewa katika Taasisi hii yanatokana na jitihada zilizofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza vifaa tiba vya matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo ili kuwawezesha wananchi wa matabaka yote kupata huduma hapa nchini.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, upasuaji mkubwa wa moyo wa kuvuna mshipa wa damu kutoka kwenye mguu na kuupandikiza katika moyo ulifanyika vizuri na hivi leo ninavyoongea kama mnavyoniona maumivu yote niliyokuwa nayo mwanzo yameacha na ninajisikia vizuri,” alisema Mhe Selelii.
Mhe. Selelii alisema kabla ya kufanyiwa upasuaji huo alianza kusikia moyo unapata vichomi maumivu ambayo yalikuwa yakienda hadi mgongoni, ni ugonjwa ambao hakuwahi kuugua katika maisha yake.
“Nilikuja Dar es Salaam kwa ajili ya mambo yangu binafsi lakini ghafla nikiwa hotelini usiku ndio nikaanza kupata maumivu ambayo yalinifanya niamke asubuhi na mapema kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu,”
“Vipimo vya awali vilionesha nina shinikizo la juu la damu la 170 kwa 120, na kushauriwa nitumie dawa za presha, baada ya kuwasiliana na ndugu na jamaa kuhusu hali niliyokutwa nayo walinishauri nifike hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Mhe Selelii.
Baada ya kufanyiwa vipimo katika hospitali ya Muhimbili ilionekana kuwa na viashiria vya magonjwa ya moyo hivyo kufikishwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya vipimo zaidi na matibabu.
“Kwakuwa sijawahi kuugua toka kuzaliwa kwangu, sikuwahi kukata bima ya afya, hivyo nilivyoambiwa nina tatizo la moyo niende JKCI niliwakatalia na kuwaambia sina hela wala bima ya afya, nashukuru wahudumu wa afya walinishawishi na kuniambia hela hutafutwa lakini maisha huwezi kuyatafuta mara ya pili hivyo ni vyema kufanyiwa uchunguzi wa kina ili ijulikane unanatizo gani,”
“Nimefurahia kwa huduma ya upasuaji wa moyo niliyoipata hapa JKCI maana waliniandaa na kuniambia kila kitu nitakachofanyiwa katika upasuaji huo na hivyo kunifanya kuwa tayari kufanyiwa upasuaji bila uoga wowote”, alizungumza kwa furaha Mhe. Selelii.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evarist Nyawawa alisema walimpokea Mhe. Selelii akiwa na matatizo ya kushindwa kupumua na kuishiwa nguvu, ambapo baada ya vipimo ilionekana mishipa mitatu ya damu inayopeleka damu katika misuli ya moyo kuziba.
“Upasuaji tuliomfanyia ni wa kuvuna mishipa ya damu kutoka katika miguu na kuipandikiza kwenye moyo, upasuaji huu umechukua masaa matano na baada kufanikisha matibabu hayo mgonjwa tulimuhamishia katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) baada ya hali yake kuimarika alipelekwa wodini na anaweza kuruhusiwa siku yoyote kuanzia sasa”, alisema Dkt. Nyawawa.
Upasuaji uliofanyika ni wa kuvuna mshipa mkubwa wa damu kutoka kwenye mguu na ndani ya kifua na kuipandikiza juu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba ili kuifanya damu iweze kupita vizuri (Coronary Artery Bypass Grafting -CABG).
Wataalamu wa magonjwa wa moyo wakiangalia maendeleo ya aliyekuwa Mbunge wa Nzega Mhe. Lucas Lumambo Selelii aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rosemary Mpella akimpima shinikizo la damu mwilini (BP) aliyekuwa Mbunge wa Nzega Mhe. Lucas Lumambo Selelii aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Picha na JKCI
No comments: