MZEE MWINYI: MKAPA ALIKUWA HANA MASIHARA KWENYE KAZI
Na Karama Kenyuko, Michuzi TV
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema Hayati Benjamin William Mkapa hakutaka masihara kwenye majukumu ya kazi jambo lililoleta manufaa kwa Taifa la Tanzania na kwa Watanzania kwa ujumla.
Mzee Mwinyi ameyasema hayo katika shughuli ya Mazishi ya Hayati Mkapa Kijijini kwao Lupaso, Mkoani Mtwara, Mzee Mwinyi amesema Hayati Mkapa alifanya kazi kuwaondolea Wananchi dhiki, matatizo na umaskini kwa kadri ya uwezo wake.
"Kwa kweli nafsi yangu imegubikwa na huzuni kama ninyi, Mzee Mkapa alifanya makubwa kwa Taifa hili na hilo ndio linatakiwa kufanywa na Kiongozi kwa Wananchi wake", amesema Alhaj Mwinyi.
Pia Mzee Mwinyi amesema Mzee Mkapa alikuwa mtu mzuri, mbaridi, amesema, wakati Rais Magufuli anachukua nchi kuongoza alikutwa ikiwa kwenye hali mbaya, lakini mwenzetu huyu, ndugu yetu amekuwa akifanya kazi ambayo sisi tulishindwa kuitengeneza ambapo moja ni kuwasaidia waja wake duniani kwa kuwaondole tabu, umasikini, dhiki na mashaka kazi iliyokuwa ya kila kiongozi.
Aidha Mzee Mwinyi amesema ameona vijana kwa wazee waliofika katika kumuaga Mzee Mkapa, wote wamevaa viatu. "Wakati wangu mimi tulikuwa tukienda popote pale miguu chini hatuna viatu, mie nimevaa viatu mara mbili, mara ya kwanza nilivaa nilipoenda jandoni na mara ya pili nikiwa nina miaka 13 nilichuma karafuu nikapata hela nikanunua viatu nikasema nitahakikisha viatu hivi haviishi, hivyo nilivifunga na kuviweka begani ili visiishe".
"Hiyo ndio kazi ya Kiongozi kuinua hadhi wananchi wake, ndivyo aliyokuwa akifanya Mkapa na anachokifanya sasa hivi Rais Magufuli. Tuendelee kumuombea asamehewe huko aendako aende huko na karatasi nyeupe isiyo na doa roho yake ipokelewe peponi.
No comments: